TANZIA-UFARANSA

RFI na France 24 zapata pigo baada ya kifo cha mwanahabari wake nguli Jean-Karim Fall

Le journaliste Jean-Karim Fall, lors d'une interview de Macky Sall pour France 24, en 2014.
Le journaliste Jean-Karim Fall, lors d'une interview de Macky Sall pour France 24, en 2014. Capture d'écran de Youtube

Shirika la habari la Ufaransa France Media Monde linalojumuisha vituo vya Redio ya RFI na televisheni ya France 24, limepata pigo baada ya kuondokewa na mmoja wa wanahabari wake nguli Jean-Karim Fall aliyefariki akiwa kwenye majukumu ya kuripoti mkutano wa wakuu wa nchi za G7 mjini Sicilya kupitia televisheni ya France 24.

Matangazo ya kibiashara

Jean-Karim Fall alikuwa mhariri mkuu na mchambuzi kwenye televisheni ya France 24 toka mwaka 2012 ambapo alijulikana kwa umahiri wake wa kuchambua habari za ulimwengu kwenye moja ya kituo kikubwa kabisa cha televisheni duniani.

Karim alikuwa maarufu pia kwa wasikilizaji wa redio hasa wapenzi wa idhaa ya RFI ambapo alianza kufanya kazi huko kati ya mwaka 1984 na 2012.

Jean-Karim alikuwa ripota wa RFI mjini Abidjan Ivory Coast na Libreville nchini Gabon na pia aliongoza idhaa ya kifaransa na alikuwa mhariri mkuu wa idhaa ya kifaransa ya RFI (Radio France International).

Mwanahabari huyu nguli atakumbukwa na wafanyakazi wenzake wa France 24 na wale wa RFI kwa namna alivyokuwa akishirikiana na wenzake hasa kwenye uchambuzi wa habari zinazohusu bara la Afrika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mashirika ya utangazaji ya France Media Monde, uongozi unatoa pole kwa familia na marafiki zake wa karibu na hasa kwa mama yake, mke wake na watoto wawili aliowaacha.

Idhaa ya RFI Kiswahili pia itamkumbuka Jean-Karim Fall kwa uchangamfu wake wakati alipoitembelea idhaa hii mwaka 2011.

Nae mkuu wa idhaa ya RFI Kiswahili Robert Minangoy amemuelezea Jean-Karim Fall kama mtu aliyekuwa tayari kusaidia wengine na mwenye moyo wa huruma, Minangoy anasema alimfahamu Jean-Karim Fall wakati akiwa kama ripota jijini Dakar na mara zote walikuwa wakizungumza habari kuhusu taifa la Senegal.

“Jean-Karim Fall ni miongoni mwa watu niliokuwa nao karibu sana alikuwa kama baba mlezi kwa mtoto wangu mwaka 1988 na alinichukua kuwa ripota wa RFI nchini Ivory Coast”.

“Sitasahau ucheshi na maneno yake ya utani na pia alikuwa mchambuzi mzuri sana wa masuala ya Afrika”. Alisema Minangoy.

Miongoni mwa wanahabari wa idhaa ya Kiswahili, Emmanuel Makundi amesema “nimeguswa na habari za kifo cha mwanahabari huyu nguli, alikuwa mcheshi na aliyekuwa tayari kukupa mawazo ya kujenga kwaajili ya taaluma ya uandishi wa habari”. Alisema mwanahabari Makundi.

Kwa upande wake mwanahabari Ali Bilali pia wa idhaa ya RFI Kiswahili alisema “nimeshtushwa sana na taarifa za kifo cha mwanahabari nguli wa televisheni ya France 24 ambaye alifariki akiwa kwenye kuripoti mkutano wa viongozi wa nchi za G7 chini Italia”.

Jean-Karim Fall amefariki akiwa na umri wa miaka 59 ambapo alizaliwa mwaka 1958. Aliishi nchini Niger ambapo baba yake Kader Fall alikuwa raia wa Senegal na waziri kwenye Serikali.

Baada ya kumaliza shule ya sekondari alienda kuishi mjini Toulouse nchini Ufaransa alikokuwa akiishi mama yake.

Alisomea masuala ya uandishi wa habari kwenye chuo cha ESJ mjini Lille kaskazini mwa Ufaransa na baadae alianza kufanya kazi na RFI baada ya kumuona ana uwezo wa kuzungumza kugha zaidi ya moja.