Familia za Chebeya na Bazana zaomba kutendewa haki DRC

Mwanaharakati wa haki za binadamu nchini DRC aliyeuawa mwaka 2010, Floribert Chebeya.
Mwanaharakati wa haki za binadamu nchini DRC aliyeuawa mwaka 2010, Floribert Chebeya. Reuters

Miaka 7 iliyopita nchini DRC, Floribert Chebeya, mwanzilishi wa shirika la kutetea Haki za Binadamu la Voix des sans voix (Sauti ya Wanyonge), alikutwa amekufa katika gari lake na dereva wake Fidèle Bazana kutoweka.

Matangazo ya kibiashara

Tarehe hii ya juni 02 leo ni miaka saba toka kuuawa kwa mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na mkuu wa Shirika la La voix des sans voix, Floribert Chebeya aliyeuawa pamoja na dereva wake Fidele Bazana, juni 02, 2010.

Kesi ya mwanaharakati huyo imesikilizwa na mahakama nchini Congo, lakini familia yake na watu wa karibu wanaona kwamba ulikuwa ni mfano wa mahakama.

Mke wake Floribert Chebeya Bi Annie Chebeya ameiambia idhaa hii ya RFI kwamba wanafanya kila linalowezekana haki itendeke.

Mwenyekiti wa shirika hilo Rostand Maketa anasema kwa sasa wameanza mchakato wa kufungua mashtaka kwenye mahakama maalum nchini Senegal, na ana imani ipo siku haki itatendeka.

Kumekuwa na utata kutokana na kifo hicho miaka saba iliyopita kwani mwili wa Chebeya ulipatikana ndani ya gari lake huku mikono yake ikiwa imefungwa, ikiwa ni siku moja baada ya kukutana na afisa mkuu wa polisi mjini Kinshasa, John Numbi.

Hadi sasa mwili wa dereva wake Fidele Bazana haujapatikana.