DRCONGO - SIASA

Familia ya Tshisekedi na serikali ya DRC zakubaliana kurejesha mwili DRC

Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa kiongozi wa upinzani nchini DRC Etienne Tshisekedi 5 janvier 2017.
Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa kiongozi wa upinzani nchini DRC Etienne Tshisekedi 5 janvier 2017. REUTERS/Francois Lenoir

Baada ya kushuhudia mvutano wa muda mrefu kati ya chama kikuu cha upinzani nchini jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na mamlaka nchini humo kuhusu eneo linalostahili kujengwa kaburi la kinara wa upinzani nchini humo Etienne Tshisekedi wa Mulumba aliyefariki dunia mjini Brussels Ubelgiji february 01 mwaka huu, hatimaye pande zote mbili zimekubaliana kuusafirisha mwili wa kinara huyo wa upinzani hadi mjini Kinshasa kwa ajili ya mazishi.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kaka wa marehemu, Gerard Mulumba, ambaye kaka yake alifariki Februari Mosi mwaka huu akipatiwa matibabu jijini Brussels Ubelgiji, amesema kuwa mwili wa Etienne Tshisekedi kutazikwa N'sele kwenye shamba la familia.

Watu walio wa karibu na kinara huyo wa upinzani walipendekeza kiongozi wao azikwe kwenye makaburi ya katikati ya mji, hususan kunako ofisi ya Limete, pendekezo hilo lilitupiliwa mbali na serikali ambayo ilitetea sheria ya mwaka 1914 ambayo inapiga marufuku kuwepo kaburi ndani ya mita 50 pembezoni mwa makazi.

Itakumbukwa kuwa eneo hilo la Nsele lilikuwa limechaguliwa tangu hapo mwanzoni na familia baada ya serikali kukataa kujengwa kaburi la Tshisekedi katikati mwa mji wa Kinshasa katika eneo la Limete.

Kaka huyo wa marehemu Gerard Mulumba ameiambia RFI kuwa wamekubaliana na serikali ya DRC kuwa mara mwili utakaposafirishwa hadi mjini Kinshasa, mwili wa Tshisekedi utapelekwa katika jumba kuu la taifa, maarufu kama palais du peuple, kuagwa kwa muda wa siku mbili kabla ya kufanyika kwa shughuli za mazishi.

Hata hivyo makubaliano hayajakamilika bado huku familia ya marehemu Tshisekedi ikisema kuwa itakutana jumapili hii, kabla ya kutangaza tarehe ya kusafirishwa mwili wa kinara huyo wa upinzani Etienne Tshisekedi.