LIBYA-SEIF AL ISLAM GADDAFI

Wapiganaji wa Zintan wamuachia mtoto wa Gaddafi, Tripoli yataka akamatwe tena

Picha ya maktaba ikimuonesha mtoto wa pili wa Gaddafi, Seif al-Islam Gaddafi akiwa kizuizini.
Picha ya maktaba ikimuonesha mtoto wa pili wa Gaddafi, Seif al-Islam Gaddafi akiwa kizuizini. REUTERS/Stringer/File Photo

Serikali iliyoko mjini Tripoli inayotambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa imepinga kuachiwa huru kwa mtoto wa pili wa Marehemu Kanali Muamar Gaddafi ikitaka mtoto huyo kukamatwa tena na kukabidhiwa kwa Serikali ya Tripoli anakotakiwa.

Matangazo ya kibiashara

Kikosi cha Abu Bakar al-Sadiq kinachoshikilia eneo la Zintan magharibi mwa nchi ya Libya, kimesema kuwa Seif al-Islam Gaddafi aliachiwa siku ya Ijumaa chini ya makubaliano ya msamaha uliopitishwa na bunge la Tobruk wakati huu wa mwezi wa Ramadhani.

Hata hivyo hakuna uthibitisho kuwa Seif al-Islam ameachiwa huru na wapiganaji hao hatua ambayo wadadisi wa mambo wanasema huenda ikazusha machafuko zaidi kwenye taifa hilo ambalo limegawanyika.

Seif al-Islam amekuwa akizuiliwa mjini Zintan toka mwezi Novemba mwaka 2011 siku chache tu baada ya baba yake kuuawa katika operesheni iliyoendeshwa na vikosi vya NATO vilivyosaidia kuunagisha utawala wake.

Al-Islam anatakiwa pia na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC kujibu mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu ambapo alihukumiwa kunyongwa na mahakama ya Tripoli.