DRC-SIASA

Koffi Annan na marais wa zamani wa Afrika wataka Uchaguzi nchini DRC kufanyika mwaka huu

Kofi Annan aliyekuwa Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Kofi Annan aliyekuwa Mkuu wa Umoja wa Mataifa REUTERS/Denis Balibouse

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan na marais saba  wa zamani wa mataifa mbalimbali barani Afrika, wametoa wito kwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuhakikisha kuwa Uchaguzi Mkuu unafanyika mwisho wa mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Annan na viongozi hao wa zamani wamesisitiza umuhimu wa rais Joseph Kabila kuhakikisha kuwa makabidhiano ya madaraka yanafanyika kwa amaani nchini humo.

Mbali na wito huo, viongozi hao wa zamani wameonesha wasiwasi wao wa kutotekelezwa kwa mkataba wa kisiasa uliotiwa saini mwaka uliopita kati ya serikali na wanasiasa wa upinzani baada ya maaskofu wa Kanisa Katoliki kufanikisha mazungumzo hayo.

Rais Joseph Kabila amekuwa akisema uchaguzi utakuwepo lakii hajasema utakuwa lini wakati huu Tume ya Uchaguzi CENI ikiendelea kuwaandikisha wapiga kura.

Hata hivyo, Annan amesisitiza kuwa hatima ya kisiasa ya DRC ipo hataraini ikiwa mkataba huo hautatekelezwa na kuwaaminisha raia kuwa uchaguzi utakaofanyika utakuwa huru na haki.

Mbali na Annan, marais wengine wa zamani waliotoa wito huo ni pamoja na Thomas BONI YAYI, rais wa zamani wa Benin, John KUFUOR,rais wa zamani wa Ghana, John MAHAMA, rais wa zamani wa Ghana, Thabo MBEKI, rais wa zamani wa Afrika Kusini.

Wengine ni Benjamin MKAPA, rais wa zamani wa Tanzania, Festus MOGAE, rais wa zamani wa Botswana, Olusegun OBASANJO, rais wa zamani wa Nigeria, Pedro PIRES, rais wa zamani wa Cape Verde na Cassam UTEEM, rais wa zamani wa Mauritius.