UN-CONGO-JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

UN: Wanajeshi 600 wa Congo Brazaville kuondolewa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wanaolinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wanaolinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati AFP PHOTO / STRINGER

Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya wanajeshi 600 kutoka nchini Congo Brazaville wanaohudumu katika jeshi lake la kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA, watarejeshwa nyumbani.

Matangazo ya kibiashara

Katibu Mkuu wa Umoja huo Antonio Guteress anatarajiwa kutangaza hatua hiyo baadaye hivi leo baada ya wanajeshi hao kubainika kuhusika katika visa vya unyanyasaji wa kingono na makosa mengine ya kinidhamu.

Kabla ya hatua hii Kamanda wa MINUSCA Luteni Jenerali Balla Keita alikuwa ameionya serikali ya Brazaville kuwarudisha nyumbani wanajeshi wake la sivyo, umoja wa Mataifa utachukua hatua.
Mwaka uliopita, wanajeshi wengine 120 kutoka Congo Brazaville walirudishwa nyumbani kwa makosa hayo ya unyanyasaji wa kingono hasa kwa watoto.

Congo Brazaville imetuma wanajeshi 629 kusaidiana na wengine katika kulinda amani nchini humo na kituo chao kimekuwa ni Berberati, mji wa tatu kwa ukubwa nchini humo.

Umoja wa Mataifa umetuma kikosi cha wanajeshi 12, 000 kulinda amani nchini humo.