AFRIKA KUSINI

Mahakama: Kura ya siri inaweza kutumiwa dhidi ya rais Jacob Zuma

Jaji Mkuu wa Afrika Kusini Mogoeng Mogoeng
Jaji Mkuu wa Afrika Kusini Mogoeng Mogoeng www.dailymaverick.co.za

Mahakama ya Juu nchini Afrika Kusini imeamua kuwa kura ya siiri unaweza kutumiwa na wabunge kupigia kura mswada wa kukosa imani na rais Jacob Zuma.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huu umekuja wakati huu rais Zuma akiendelea kukabiliwa na shinikizo za kujiuzulu kwa madai ya kushiriki katika kashfa mbalimbali za ufisadi na kuathiri uchumi wa nchi hiyo.

Jaji Mkuu Mogoeng Mogoeng amesema kuwa Spika wa bunge ana uwezo wa kikatiba kuamuru wabunge kupiga kura ya siri kuamua hatima ya rais Zuma.

Chama cha upinzani DA kilikwenda Mahakamani kutaka uamuzi huo kufanyika baada ya kuwasilisha mswada wa kukosa imani na rais Zuma baada ya kudai kuwa baadhi ya wabunge wa ANC walikuwa tayari kuunga mkono kuondolewa kwa Zuma lakini wana wasiwasi kuwa watafahamika.

Hata hivyo, haijafahamika ni lini mswada huo utajadiliwa na kupigiwa kura bungeni.

Mbali na maandamano ya kumtaka kujiuzulu, Zuma pia amekuwa akishtumiwa kumfuta kazi aliyekuwa Waziri wa Fedha Pravin Gordhan aliyekuwa anapambana na ufisadi.

Rais Zuma, amekanusha madai hayo yote na amekuwa akinukuliwa akisema chama chakecah ANC  kikiamua asiwe kiongozi, ataondoka.