AFRIKA KUSINI-ZUMA_UFISADI

Upinzani wakaribisha uamuzi wa mahakama kuruhusu kura ya siri dhidi ya Zuma

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma aendelea kukabiliwa na shinikizo za kujiuzulu kwa madai ya kushiriki katika kashfa mbalimbali za ufisadi na kuathiri uchumi wa nchi.
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma aendelea kukabiliwa na shinikizo za kujiuzulu kwa madai ya kushiriki katika kashfa mbalimbali za ufisadi na kuathiri uchumi wa nchi. Reuters/Rogan Ward

Nchini Afrika Kusini, upinzani wa kisiasa umesema kuridhika kufuatia uamuzi wa mahakama ya nchi hiyo kuruhusu kura ya siri ya kutokua na imani na rais wa nchi hiyo Jacob Zuma.

Matangazo ya kibiashara

Siku ya Alhamisi, Juni 22, mahakama ya juu zaidi nchini Afrika Kusini iliruhusu Bunge kupitisha kura ya siri ya kutokuwa na imani dhidi ya rais Jacob Zuma.

Uamuzi huu umekuja wakati huu rais Zuma akiendelea kukabiliwa na shinikizo za kujiuzulu kwa madai ya kushiriki katika kashfa mbalimbali za ufisadi na kuathiri uchumi wa nchi hiyo.

Vyama sita vya upinzani viliiomba mahakama kuruhusu kura ya siri dhidi ya rais Jacob Zuma, wakiamini kwamba baadhi ya wabunge wa vyama vinavyunga mkono serikali, waliochoshwa na kiongozi wao, wataunga mkono kura hii ya kutokuwa na imani na kiongozi huyo.

Spika wa Bunge ana mamlaka ya kuitisha kikao cha kupiga kura ya siri ya kutokua na imani dhidi ya rais nchi hiyo. Hadi sasa, kiongozi huyo wa Taasisi hii ya Bunge ambaye ni mshirika wa karibu wa rais Zuma amepinga hoja hii, akisema kuwa haruhusiwi. Mahakama ya juu ya Afrika Kusini imemnyooshea kidole cha lawama. Na kumkumbusha kwamba uamuzi wake unapaswa kuchukuliwa kwa maslahi ya demokrasia.