DRC-AFRIKA KUSINI

Kabila: Tutaendelea kuzungumzia hali ya kisiasa kufikia mwafaka

Rais wa DRC  Jospeh Kabila (Kushoto) akiwa na mwenyeji wake rais Jacob Zuma (Kulia) baada ya kumtembelea Juni 25 2017 jijini Pretoria
Rais wa DRC Jospeh Kabila (Kushoto) akiwa na mwenyeji wake rais Jacob Zuma (Kulia) baada ya kumtembelea Juni 25 2017 jijini Pretoria

Afrika Kusini inaitaka serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na wanasiasa wa upinzani kuendelea kuzungumza ili kupata mwafaka wa kisiasa katika taifa hilo la Afrika ya Kati.

Matangazo ya kibiashara

Kauli hii imetolewa na rais Jacob Zuma baada ya kukutana na nwenyeji wake rais Joseph Kabila jijini Pretoria.

Zuma amesema ameridhishwa na kufurahishwa na makubaliano ya kisiasa yaliyofikiwa na kutiwa saini mwezi Desemba mwaka uliopita kati ya serikali na upinzani.

Kabila amesema serikali yake itaendeleza mazungumzo ya kisiasa mara kwa mara kufanikisha uongozi bora na amani nchini humo.

“Mazungumzo nchini DRC yataendelea kwa muda mrefu. Tutayatumia kama njia ya uongozi,” amesema.

Aidha, ameleeza kuwa lengo la mazungumzo haya ni kufanikisha kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu nchini humo, zoezi ambalo hajasema ni lini litafanyika.

Wapinzani wameendelea kulaani uongozi wa Kinshasa, kwa kukataa kutekeleza mkataba wa kisiasa na kufanyika kwa uchaguzi Mkuu kwa madai kuwa rais Kabila hataki kuondoka madarakani.

Kutotekelezwa kikamilifu kwa mkataba huo, kumechelewesha pia kuzikwa kwa kiongozi wa upinzani Ettiene Tshisekedi aliyefariki dunia mwezi Februari mwaka huu.