DRC-SIASA

Mkuu wa Tume ya Uchaguzi nchini DRC asema Uchaguzi hauwezi kufanyika Desemba

Rais wa Tume ya Uchaguzi nchini DRC, Corneille Nangaa  Yobeluo (Katikati), akizungumza hivi karibuni akiwa mjini Goma
Rais wa Tume ya Uchaguzi nchini DRC, Corneille Nangaa Yobeluo (Katikati), akizungumza hivi karibuni akiwa mjini Goma MONUSCO/Alain Wandimoyi

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Corneille Nangaa amesema Uchaguzi Mkuu nchini humo hauwezi kufanyika mwezi Desemba au kabla ya mwezi huo mwaka huu kama ilivyopangwa.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza jijini Paris, Nangaa amesema sababu kubwa inayofanya Uchaguzi huo kutofanyika kama ilivyopangwa ni utovu wa usalama katika jimbo la Kasai.

Mwenyekiti huo ameongeza kuwa, jitihada zinafanyika, kuhakikisha kuwa wakaazi wa kasai wanasajiliwa kama wapiga kura kuanzia mwezi ujao.

Mkataba wa kisiasa uliofikiwa mwezi Desemba mwaka uliopita, ulitaka Uchaguzi kufanyika mwezi Desemba na rais Joseph Kabila kutowania.

Rais Kabila mwenye amekuwa akisema Uchaguzi utafanyika nchini humo lakini hajawahi kusema utafanyika lini.

Wanasiasa wa upinzani nchini humo wamekuwa wakisema kuwa rais Kabila anachelewesha makusudi mchakato wa maandalizi ya Uchaguzi ili kuendelea kukaa madarakani.

Umoja wa Mataifa umekuwa ukiitaka Tume ya Uchaguzi nchini humo kutangaza kalenda ya Uchaguzi, na kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unafanyika mwaka huu kama ilivyopangwa.

Hata hivyo, CENI imekuwa ikisema kuwa Tume ya Umoja wa Mataifa haiwezi kuipangia kazi yake.