DRC-MONUSCO-USALAMA

Kiongozi wa kivita DRC ajisalimisha kwa MONUSCO

Kiongozi wa kivita Sheka Ntabo Ntaberi katika mkutano wa mwezi Novemba 2011 (picha ya zamani).
Kiongozi wa kivita Sheka Ntabo Ntaberi katika mkutano wa mwezi Novemba 2011 (picha ya zamani). STR / AFP

Kiongozi wa kivita Ntabo Ntaberi, anaetuhumiwa kuhusika kwa kampeni kubwa ya ubakaji katika mji wa Walikale mwaka 2010 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, alijisalimisha Jumatano hii asubuhi kwa kikosi cha Umoja wa mataifa nchini humo MONUSCO.

Matangazo ya kibiashara

Hati ya kukamatwa dhidi Ntabo Ntaberi ilitolewa mnamo mwaka 2011 na mahakama ya kijeshi ya DRC. Tangu wakati huo alishtumiwa na mashirika ya haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na Human Rights Watch, kuua raia kadhaa.

Alipoteza wapiganaji wake wengi wakati wa kuwania kuongoza kwa mara ya pili kundi hilo la waasi.Taarifa ya kujisalimisha kwake imethibitishwa na msemaji wa tume ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ntabo Ntaberi alijisalimisha katika eneo la Mutongo katika mji wa Walikale na alisafirishwa mjini Goma na Umoja wa Mataifa. Atazuiliwa kwa muda wa siku kadhaa, kwa uchunguzi wa afya kabla ya kukabidhiwa kwa mamlaka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.