ZAMBIA-DRC-WAKIMBIZI-USALAMA

UNHCR yatiwa wasiwasi na maelfu ya wakimbizi wa DRC nchini Zambia

Mji wa Lusaka, mji mkuu wa Zambia. (Picha ya Zamani).
Mji wa Lusaka, mji mkuu wa Zambia. (Picha ya Zamani). © Getty Images/Stuart Fox

Tangu Agosti 30, zaidi ya raia 3,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamekimbia mikoa ya Tanganyika na Haut-Katanga mashariki mwa DRC.

Matangazo ya kibiashara

Maelfu ya wakimbizi hao wamekimbilia nchini Zambia. Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi (UNHCR0 linasema lina wasiwasi mkubwa na wingi wa wakimbizi hao.

Raia hawa wanakimbia mapigano kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo wenye silaha na wamekua wakiwasili nchini Zambia wakiwa katika hali mbaya ya afya. Wamekimbia machafuko makubwayanayoendelea kuripotiwa katika maeneo hayo, amesema Katerina Kitidi, msemaji wa UNHCR mjini Geneva:

"Ni idadi kubwa sana ya wakimbizi. Katika siku moja, tarehe 30 Agosti, zaidi ya watu 600 waliingia nchini Zambia. Hali bado ni ya wasiwasi kwa sababu watu hawa wanatoa ushuhuda wa habari ambazo ni za ukatili sana.

Wanazungumzia mauaji, ubakaji, uporaji. Wana mahitaji makubwa. Wengi wao ni wanawake na watoto. Tunaona watoto wengi. Wakati mwingine wanaonekana na ishara za utapiamlo. Wanakabiliwa na malaria, maambukizi ya kupumua, kuhara, magonjwa ya ngozi. Wanahitaji msaada wa dharura, ulinzi, ikiwa ni pamoja na chakula na maji, na usafi wa mazingira. "

UNHCR inaomba dola milioni 3.5 ili kukidhi mahitaji ya wakimbizi hawa, kwa kuwa Zambia imekuwa tayari kuwahudumia wakimbizi 26,000 wa DR Congo.