Upinzani DRC wafutilia mbali kuahirishwa kwa uchaguzi hadi mwaka 2019
Imechapishwa:
Upinzani nchini nchini DRC umesema kauli ya tume ya uchaguzi CENI kwamba uchaguzi mkuu nchini humo hautafanyika kabla ya mwaka 2019, ni kama kutangaza vita dhidi ya wananchi.
Kinara wa upinzani Felix Tshisekedi amesema kauli ya CENI haikubaliki.
Naye katibu mkuu wa chama cha Upinzani cha MLC Bi eve Bazaiba amesema kauli ya CENI ni utapeli, na inazua sintofahamu zaidi ya kiusalama kuhusu mustakabali wa siasa za nchi hiyo.
Serikali inasema bado inatafakari kuhusu tangazo hilo, kama anavyoeleza Lambert Mende msemaji wa serikali ya Kinshasa,
Kwa mujibu wa makubaliano ya kisiasa yaliyosimamiwa na baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki na kutiwa saini na wanasiasa nchini DRC, uchaguzi mkuu ulipaswa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu kuchukua nafasi ya rais Joseph Kabila aliyemaliza muda wake.
Hivi sasa tume ya uchaguzi inasema itahitaji siku nyingine 504 kuandaa uchaguzi mwingine baada ya kumaliza zoezi la uandikishaji wapiga kura.