ZIMBABWE-UCHAGUZI-SIASA-USALAMA

Rais Mugabe na familia yake haijulikani waliko

Magari ya kijeshi yakiegeshwa nje kidogo ya mji wa Harare, Novemba 14, 2017.
Magari ya kijeshi yakiegeshwa nje kidogo ya mji wa Harare, Novemba 14, 2017. REUTERS/Philimon Bulawayo

Hali ya sintofahamu inaendelea kushuhudiwa nchini Zimbabwe, baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa madaraka tangu usiku wa Jumanne kuamkia Jumatano hii.

Matangazo ya kibiashara

Mpaka sasa haijulikani aliko rais Robert Mugabe na familia yake, licha ya baadhi ya taarifa zinasema kuwa mkewe Mugabe, Grace Mugabe huenda alitorokea Namibia.

Hakujakuwa na tamko lolote kutoka kwa serikali kuhusu yanayojiri, jambo ambalo linaashiria kwamba huenda ni kweli Mugabe na watu wake hawana udhibiti tena wa serikali.

Na kwa sasa hakuna taarifa zozote kwamba kikosi cha walinzi wa Rais Mugabe, ambacho humtii Bw Mugabe, kimejaribu kuingilia kati.

Inaripotiwa kuwa baadhi ya mawaziri hasa wale ambao ni washirika swa karibu wa Bw Mugabe, wanashikiliwa na jeshi.

Awali jeshi lilitangaza kwamba linawatafuta wahalifu walio karibu na Rais Mugabe.

Inaonekana kana kwamba hatua ya jeshi imechochewa na kufutwa kwa makamu wa rais Emmerson Mnangagwa jumalililopita.

Bw Mnangagwa amekuwa mpinzani mkuu wa Grace Mugabe, mkewe Rais Mugabe.

Emmerson Mnangagwa ni wa kizazi cha wazee ambao waliongozwa vita vya ukombozi nchini Zimbabwe miaka ya 1970 na kuchangia uhuru wa Zimbabwe kutoka kwa Uingereza mwaka 1980 ambapo Mugabe aliongoza akiwa waziri mkuu na baadaye kama rais.

Jumatatu, Jenerali Chiwenga alitishia kwamba operesheni ya kuwaondoa wanaompinga rais katika chama tawala inafaa kusitishwa la sivyo jeshi lingeingilia kati.

Mpaka sasa haijajulikana hasara ambayo imetokea tangu hali hiyo ianze, ambapo milipuko na milio ya risasi ilisikika usiku wa kuamkia Jumatano hii karibu na majengo ya serikali katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare.