DRC-MGOMO-SIASA-USALAMA

Vyama vya kiraia DRC vyaitisha mgomo wa kitaifa

Tume ya Umoja wa Mataifa nchini DRC (MONUSCO) imeiomba serikali ya DRC kuheshimu haki ya kuandamana. ( hapa kwenye picha makao makuu ya serikali, Kinshasa).
Tume ya Umoja wa Mataifa nchini DRC (MONUSCO) imeiomba serikali ya DRC kuheshimu haki ya kuandamana. ( hapa kwenye picha makao makuu ya serikali, Kinshasa). JUNIOR KANNAH/AFP

Vyama vya kiraia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimeitisha mgomo wa kitaifa hivi leo Jumatano kupinga kalenda ya uchaguzi na kushinikiza utekelezwaji wa mkataba wa kisiasa uliotiwia saini kati ya upinzani na vyama vinavyounga mkono serikali mwezi Desemba mwaka 2016.

Matangazo ya kibiashara

Wafanyikazi wa serikali na wale kutoka sekta za kibinafsi wametakiwa kusalia nyumbani Jumatano hii kuonesha masikitiko yao kuhusu utekelezwaji wa mkataba huo na kuunga mkono jitihada za upinzani.

Kundi moja la muungano wa upinzani wa Rassemblement linaloongozwa na mtoto wa EtienneTshisekedi, Felix Tshisekedi, lilisema jana katika mkutano na waandishi wa habari mjini Kishasa kwamba linaunga mkono mgomo huo.

"Rassemblement inaunga mkono vitendo vyote vitakavyoenda katika mwelekeo wa kuwaita watu wetu kuzuia barabara, kwa mujibu wa Ibara ya 64 ya katiba, kwa mtu binafsi au kundi la watu ambao leo wameiteka DR Congo na wanataka kulazimisha utawala wa kiimla kwa muda mrefu unaopingwa nchini humu, "alisema Felix Tshisekedi.

Mkutano wowote wapigwa marufuku

"Mkutano wowote wa watu zaidi ya 5 utatawanywa bila huruma," ameonya Kamishna wa polisi wa mkoa Kinshasa, Sylvano Kasongo.

Akijibu kuhusu taarifa ya Tume ya Umoja wa Mataifa (MONUSCO), Jenerali Sylvano Kasongo amesema: "DRC haishinikizwi na MONUSCO. DRC ni nchi huru. Polisi inatekeleza amri kutoka viongozi wa siasa na utawala na sio MONUSCO. "

Tume ya Umoja wa Mataifa nchini DRC (MONUSCO) ulitoa wito wa kuheshimu haki ya kuandamana kwa kwa utulivu na kujizuia. Wakati huo huo, ilihimiza serikali ya DRC kuheshimu haki ya msingi kama inavyoelezwa kwenye Katiba ya nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na uhuru wa mikutano na maandamano, na kufundisha vikosi vya ulinzi na usalama kuheshimu kanuni muhimu, uwiano na uhalali, kulingana na viwango vya kimataifa.

"Sisi, tunaheshimu agizo la Gavana. Gavana alituagiza kutawanya maandamano ya hapo kesho, "alisema Jenerali Sylvano Kasongo.

Hivi karibuni Tume ya Uchaguzi nchini DRC ulitangaza kalenda ya uchaguzi na kusema kuwa uchaguzi umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka ujao.