ZIMBABWE-SIASA-USALAMA

Jeshi lachukua udhibiti Zimbabwe

Upinzani hafifu wajitokeza katika jeshi la Zimbabwe
Upinzani hafifu wajitokeza katika jeshi la Zimbabwe REUTERS/Philimon Bulawayo

Hali ya sintofahamu yaendelea kushuhudiwa nchini Zimbabwe, ambapo jeshi limedhibiti maeneo kadhaa muhimu pamoja na majengo ya serikali. Baadhi ya mawaziri wamewekwa chini ya ulinzi.

Matangazo ya kibiashara

Rais Robert Mugabe amewekwa chini ya kifungo cha nyumbani na mkewe Grace Mugabe, ambaye ni mmoja wa wahusika wakuu wa mgogoro huo wa kisasia, anaripotiwa kutorokea nchini Namibia. Hata hivyo jeshi bado linakataa kuzungumzia iwapo ni mapinduzi ya kijeshi yanayoendelea.

Jumuiya ya kimataifa imetoa wito kwa pande husika kujizuia na kurejea kwa hali ya utulivu nchini Zimbabwe.

Uingereza kupitia waziri wake wa Mambo ya Nje Boris Johnson, imeonya kuhusu "serikali ya mpito ambayo itaongozwa na mtu ambaye hakuchaguliwa na raia".

"Tunaangalia kwa makini hali inayoendelea nchini Zimbabwe. Hali bado ni tate, "Waziri Mkuu Theresa May aliwaambia Wabunge wa Uingereza kabla ya kutoa wito " kwa pande zote kujizuia na machafuko".

Waziri wa Mambo ya Nje Boris Johnson pia ameomba "utulivu na kujizuia" mbele ya Bunge. "Hatujui vipi hali hiyo itaendelea katika siku zijazo au iwapo inaashiria kuanguka au la kwa utawala wa Mugabe."

Umoja wa Umoja wa Mataifa na Marekani watoa wito kwa pande husika kujizuia na machafuko

"Serikali ya Marekani ina wasiwasi kuhusu hatua ya hivi karibuni ya jeshi la Zimbabwe," afisa mmoja wa Marekani ameliambia shirika la habari la AFP. "Marekani haitaki kuingilia masuala ya ndani ya siasa ya Zimbabwe," lakini, kwa uhahika, "hawakubaliani na kuingilia kijeshi katika michakato ya kisiasa," aliongeza.

"Tunatoa wito kwa viongozi wote wa Zimbabwe kujizuia, kuheshimu utawala wa sheria na haki za wananchi wote wanaolindwa na Katiba, na kutatua migogoro haraka ili kuwezesha kurudi haraka kwa hali ya kawaida", afisa huyo amesema..

Alikumbusha kuwa ubalozi wa Marekani mjini Harare ulikuwa umewahimiza raia wa Marekani kusalia nyumbani.

Guterres aomba pande husika kujizuia na machafuko

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameomba "utulivu na kujizuia na machafuko," amesema Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq. "Ninawaomba kufadhi haki ya msingi, ambayo ni uhuru wa kujieleza na mkusanyiko ni muhimu sana," Bw Guterres amesema, kwa mujibu wa msemaji huyo. Kwa mujibu wa antonio Guterres, "tofauti za kisiasa zinapaswa kutatuliwa kwa amani na kupitia mazungumzo, kwa mujibu wa katiba ya nchi," bW Haq ameongeza.

Umoja wa Ulaya (EU) waatarajia "azimio la amani"

Umoja wa Ulaya umesema una wasiwasi kuhusu hali inayoendelea nchini Zimbabwe, huku ikitoa wito kwa "mazungumzo" kwa "azimio la amani".

"Tunatoa wito kwa pande zote vinazohusika kuachana na malumbano na kuweka mbele mazungumzo kwa lengo la azimio la amani," msemaji wa Tume ya moja wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ray, amesema katika mkutano na vyombo vya habari.

Umoja wa Afrika watoa wito wa "kuheshimu Katiba"

Mkuu wa Umoja wa Afrika (AU) amesema yanayojiri nchini Zimbabwe ni 'kama mapinduzi'.

Alpha Conde, ambaye ni rais wa Guinea, pia rais wa Umija wa Afrika (AU) amesema kilichotokea Zimbabwe bila shaka ni "wanajeshi kujaribu kuchukua mamlaka kwa nguvu".

Mkuu huyo wa Umoja wa Afrika (AU) ametoa wito kwa jeshi kukomesha wanalofanya - jambo ambalo amesema "linaonekana kama mapinduzi ya serikali", kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

Hilo linakinzana na msimamo wa jeshi la Zimbabwe ambalo limesisitiza kwamba halijatekeleza mapinduzi ya kijeshi, bali linajaribu kuwaondoa "wahalifu" wanaomzingira Rais Mugabe.

Zuma aitisha mkutano Gaborone

Siku ya Jumatano mchana Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, mshirika wa karibu wa Robert Mugabe aliongea kwa simu mkongwe huyo wa uhuru wa Zimbabwe na alihakikisha kwamba yuko chini ya kifungo cha nyumbani.

Jacob Zuma, ambaye alisema "ana wasiwasi" ana hali inayoendelea Zimbabwe, aliwatuma mawaziri wake wawili mjini Harare kwa niaba ya Jumuiya ya nchi za kusini mwa ukanda wa Afrika (SADC) anayoongoza. Wajumbe hawa wawili wa rais wa Afrika Kusini wawasili Harare. Wanatazamiwa kukutana na kiongozi wa zamani wa uhuru na viongozi wa jeshi, wakisubiri mkutano utakaofanyika Alhamisi alasiri mjini Gaborone.