CAMEROON-VYOMBO VYA HABARI

Kesi ya Ahmed Abba nchini Cameroon: Mahakama kutoa uamuzi wake Desemba 21

Ahmed Abba (picha ya zamani).
Ahmed Abba (picha ya zamani). © RFI

Mahakama ya Rufaa ya kijeshi nchini Cameroon ilimsikiliza mwandishi wa habari wa RFI katika lugha ya Hausa nchi humo, ambaye alifutiwa katika mahakama ya mwanzo kosa la ugaidi na kumhukumu miaka 10 jela kwa kutotoa taarifa kwa ngazi husika na kupokea fedha kutoka kundi la kigaidi.

Matangazo ya kibiashara

Kesi itakayofuata itakua ya mwisho katika kesi hiyo inayodumu miaka miwili na nusu na uamuzi wa mahakama unatarajiwa Desemba 21.

Kesi hii ilianza kusikilizwa Alhamisi mchana na kumalizika usiku baada ya malalamiko ya wanasheria wa upande wa utetezi. Hali hiyo ilipelekea mahakama kufuta undani wa kesi hiyo, kusikiliza pande zote, ikiwa ni pamoja na Ahmed Abba.

Wakati wa kesi hiyo, mwandishi wa RFI alirejelea hali iliyomsibu wakati wa kukamatwa kwake katika mji wa Maroua Julai 30, 2015, ikifuatiwa na kufungwa kwake katika idara mbalimbali za polisi kati ya Maroua na Yaounde. Alielezea mateso aliopata, huku akibaini kwamba alifungwa mahali pasipojulikana kwa siku 90.

Mwendesha mashitaka aliomba mahakama kuthibitisha hukumu ya mahakama ya mwanzo ya kifungo cha miaka 10.

Wanasheria wa Ahmed Abba walifutilia mbali madai ya mwendesha mashitaka na kueleza kwamba hakuna ushahidi aliotoa wa kuonyesha kuwa Ahmed Abba alihusika kwa makosa hayo anayoshtumiwa na kuomba achiliwe huru mara moja.

Mahakama Kuu inatazamia kutoa uamuzi wake Desemba 21.