ZIMBABWE

Hali ya sintofahamu yaendelea Zimbabwe , maandamano zaidi yapangwa

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe akionekana kwa mara ya kwanza hadharani  17 Novemba 2017.
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe akionekana kwa mara ya kwanza hadharani 17 Novemba 2017. REUTERS/Philimon Bulawayo

Zimbabwe hii leo imejikuta katika mkwamo zaidi huku maandamano yakipangwa wakati huu wakongwe wa vita vya uhuru, wanaharakati na viongozi wa chama tawala ZANU PF wakitoa wito hadharani kwa Rais Robert Mugabe kulazimishwa kung'atuka mamlakani.

Matangazo ya kibiashara

Maandamano hayo yatakamilisha juma ambalo maafisa wa jeshi walichukua mamlaka na kumweka rais Robert Mugabe chini ya kizuizi nyumbani kwake katika mabadiliko ya kushangaza dhidi ya rais Mugabe ambaye amewala tangu 1980

Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 93 hakujiuzulu katika mazungumzo na mkuu wa jeshi siku ya Alhamisi na vyanzo vinasema kuwa kiongozi huyo mkongwe bado anaendelea kutafakari kujadili mwisho wa utawala wake wa miaka 37.

Mugabe alionekana hadharani kwa mara ya kwanza katika maandalizi ya sherehe ya kuhitimu masomo ya chuo kikuu huko Harare siku ya Ijumaa, na kuacha maswali zaidi kuhusu hali ya mazungumzo yake na Generali Constantino Chiwenga, ambaye aliongoza udhibiti wa kijeshi.

Baadaye mchana, matawi nane kati ya kumi ya chama tawala cha rais Mugabe walionekana katika televisheni wakimtaka aachie madaraka.

Cornelius Mupereri, msemaji wa ZANU -PF katika mkoa wa Midlands ,ni mmoja wa viongozi kadhaa wa chama walioonekana katika televisheni ya ZBC akisoma taarifa zinazofanana za kumtaka rais Mugabe kung'atuka.