ZIMBABWE

Mugabe na wakuu wa jeshi kusaka ufumbuzi wa mzozo katika mazungumzo ya jumapili

Raisi wa Zimbabwe Robert Mugabe akiwa Harare Nov 17 2017
Raisi wa Zimbabwe Robert Mugabe akiwa Harare Nov 17 2017 REUTERS/Philimon Bulawayo

Raisi wa Zimbabwe Robert Mugabe atakutana na wakuu wa jeshi leo jumapili kwa lengo la kumaliza mzozo ulioibuka juma lililopita.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa ZBC raisi Mugabe atakutana na Mkuu wa jeshi mteule na Padri Fidelis Mukonori wa kanisa katoliki ambaye anasimamia mazungumzo hayo kati ya jeshi na raisi.

Aidha chanzo kimoja kutoka ndani ya chama tawala ZANU PF kimedokeza kuwa leo kitafanya mkutano wa kujadili hatma ya kiongozi huyo.

Tangazo hilo linakuja baada ya kushuhudia maandamano ya wazimbabwe nchini humo na jijini London wakidai kuondoka madarakani kwa kiongozi huyo mkongwe ambaye amekuwa mamlakani kwa takribani miaka 40.

Maandamano ya umma yamekuja baada ya juma lililoshuhudia jeshi likidhibiti nchi hiyo na kumzuia nyumbani raisi Mugabe baada kufutwa kazi kwa makamu wake Emmerson Mnangagwa.