ZIMBABWE

ZANU-PF yamchagua Mnangagwa, yamtaka Mugabe kuachia ngazi kabla ya Jumatatu mchana

Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe
Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe REUTERS/Mike Hutchings

Chama tawala nchinik Zimbabwe ZANU-PF kimetangaza rasmi kumvua nafasi yake rais Robert Mugabe kama mwenyekiti wa chama na kumteua aliyekuwa makamu wake wa rais Emmerson Munangagwa kuwa mwenyekiti wa muda.

Matangazo ya kibiashara

Chama hicho pia kimemfuta uanachama mke wa rais Mugabe, Grace Mugabe kwa kile chama hicho kimesema ni kuonesha kiburi na tabia za utovu wa nidhamu dhidi ya viongozi wa juu wa chama.

Kwenye taarifa yao baada ya mkutano maalumu wa chama uliofanyika mjini Harare, waziri wa masuala ya mtandaoni Patrick Chinamasa, amesema kamati ya uongozi ya chama imeridhia kwa kauli moja kumuondoa kwenye nafasi yake rais Mugabe kama kiongozi wa chama.

Chinamasa ameongeza kuwa kutokana na uamuzi huo, kamati ya utendaji imeridhia na kumrejesha kwenye chama aliyekuwa makamu wake wa rais Emmerson Munangagwa aliyefukuzwa na rais Mugabe takribani majuma mawili yaliyopita.

Waziri Chinamasa mbali na kumrejesha Mnangagwa pia ametangaza kuondolewa kwenye nafasi yake makamu wa rais wa chama hicho pamoja na wanachama wengine ambao walikuwa wanawalinda wahalifu ndani ya chama.

Kwenye taarifa yake ZANU-PF imempa makataa ya hadi kufikia siku ya Jumatatu mchana kwa rais Mugabe kuwa ameondoka madarakani kwa hiari yake ama sivyo ataondolewa kwa nguvu kupitia bunge.

Ikiwa rais Mugabe hatakuwa amejiuzulu nafasi yake mpaka kufikia kesho mchana, basi chama hicho kimemuagiza kiongozi wa waliowengi kwenye bunge kuwasilisha muswada rasmi wa kutokuwa na imani na rais Mugabe na kupiga kura ya kumuondoa kama rais.

Uamuzi huu unamaanisha kuwa utawala wa karibu miaka 37 madarakani wa rais Mugabe unatamatika rasmi baada ya juma moja lililopita pia kushuhudia jeshi likishika hatamu na kumuweka kizuizini kwenye makazi yake.

Uamuzi huu wa chama unamaanisha pia kuwa katika uchaguzi wa mwaka ujao, chama hicho kinamteua Emmerson Mnangagwa kuwa mgombea wake wa kiti cha urais.

Rais Mugabe ambaye anasalia kuwa kiongozi mkongwe zaidi duniani, bado anasalia kuwa rais wa taifa lakini sasa anapata upinzani mkali kutoka kwa viongozi wa juu wa jeshi, wananchi na hata wafuasi wa chama hicho.

Mkuu wa majeshi ambaye ameongoza operesheni za juma lililopita anaendelea na mazungumzo na rais Mugabe ambapo matokeo ya kikao chao yanatarajiwa kutangazwa muda wowote kuanzia sasa.