Hatma ya Robert Mugabe mashakani

Waandamanaji wakimtaka Rais Robert Mugabe kujiuzulu, Harare, mji mkuu wa Zimbabwe, Novemba 18, 2017.
Waandamanaji wakimtaka Rais Robert Mugabe kujiuzulu, Harare, mji mkuu wa Zimbabwe, Novemba 18, 2017. REUTERS/Philimon Bulawayo

Hali ya sintofahamu inaendelea nchini Zimbabwe, baada ya rais Robert Mugabe kuapa kutoachia madaraka katika hotuba yake kwa taifa siku ya Jumapili usiku.

Matangazo ya kibiashara

Wakati huo huo jeshi linatarajiwa kuwa na mkutano na waandishi wa habari Jumatatu hii asubuhi pamoja na Muungano wa Wapiganaji waliopigania Uhuru wa Zimbabwe.

Katika hotuba yake ya kwanza kwa taifa tangu jeshi lichukue madaraka Jumatano, Mugabe hakujiuzulu na alisema kuwa ameazimia kuongoza kongamano lijalo la Zanu-PF.

Mamlaka ya Mugabe yalidhoofishwa tangu jeshi lilipoingilia kati siku Jumatano Novemba 15, wakati ulipoibuka mzozo juu ya nani anayepaswa kumrithi.

Mzozo huo uliibuka wiki mbili zilizopita wakati rais Mugabe alipomfuta kazi makamu wake Emmerson Mnangagwa, jambo lililowakasirisha maafisa waaandamizi wa jeshi , ambao waliona kuwa ni shinikikizo kutoka kwa mkewe Grace Mugabe kutaka amrithi mumewe kwenye uongozi wa nchi.

Haijafahamika kwamba bunge litaanza mchakato wa kumtimua mamlakani. Siku ya Jumapili mkutano wa dharura wa chama cha Zanu-PF ulitoa muda wa makataa wa Robert Mugabe kujiuzulu kabla ya Jumatatu saa sita mchana.