ZIMBABWE

Robert Mugabe ajiuzulu kama rais wa Zimbabwe

Robert Mugabe wakati akiwa rais wa Zimbabwe
Robert Mugabe wakati akiwa rais wa Zimbabwe REUTERS/Philimon Bulawayo

Robert Mugabe ajiuzulu kama rais wa Zimbabwe. Tangazo hili limetolewa na Spika wa bunge Jumanne jioni Jacob Mudenda kwa wabunge waliokuwa wameanza kujadili mswada wa kukosa imani na kiongozi huyo.

Matangazo ya kibiashara

Mugabe anaondoka madarakani baada ya kuongoza nchi hiyo kwa miaka 37 tangu mwaka 1980, wakati nchi hiyo ilipopata uhuru.

“Mimi Robert Mugabe, kwa mujibu wa kifungu cha 96 cha Katiba ya Zimbabwe natangaza kujiuzulu mara moja,” alisema Spika Mudenda.

Kujiuzulu kwa Mugabe, kumeleta furaha kubwa nchini humo hasa jijini Harare kwa maelfu ya wananchi kujitokeza kusherehekea ushindi huu.

Wabunge wa Zimbabwe wakishangilia hatua ya Mugabe kujiuzulu, Harare Novemba 21, 2017.
Wabunge wa Zimbabwe wakishangilia hatua ya Mugabe kujiuzulu, Harare Novemba 21, 2017. Jekesai NJIKIZANA / AFP

Raia wa Zimbabwe wanaamini kuwa, kujiuzulu kwa Mugabe ni mwamko mpya kwa nchi yao kiuchumi na kisiasa.

Makamu wa rais wa zamani Emmerson Mnagangwa, anatarajiwa kuongoza kwa muda kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka ujao.

Jeshi nchini humo lilianzisha mchakato wa kukosa imani na uongozi wa Mugabe baada ya mkewe Grace, kuonekana kuingilia uongozi wake.

Baada ya tangazo la kujiuzulu kwa Mugabe wananchi wa Zimbabwe walimiminika katika mitaa ya miji mbalimbali nchini humo kusherehekea hatua hiyo.