MALI-UN-USALAMA

Askari watatu wa Umoja wa Mataifa wauawa kaskazini mwa Mali

Kikosi cha askari wa Umoja wa Mataifa nchini Mali (Minusma) kinaendelea kukabiliana makundi yenye silaha.
Kikosi cha askari wa Umoja wa Mataifa nchini Mali (Minusma) kinaendelea kukabiliana makundi yenye silaha. SEBASTIEN RIEUSSEC / AFP

Askari wasiopungua watatu wa Umoja wa Mataifa (Minusma) na mmoja wa Mali wameuawa leo Ijumaa katika shambulizi lililotokea kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

"leo asubuhi, kikosi cha Umoja wa Mataifa (Minusma )kilifaulu kuzima shambulio wakati wa operesheni ya pamoja na FAMas (vikosi vya jesji la Mali) katika mkoa wa Menaka", kwa mujibu wa taarifa ya Minusma.

"Askari watatu wa Minusma waliuawa, wengine kadhaa walijeruhiwa, baadhi wakiwa katika hali mbaya, na askari mmoja wa Mali aliuawa na mmoja alijeruhiwa, Minusma imebaini.

Washambuliaji kadhaa pia waliuawa, na wengine walijeruhiwa, kulingana na chanzo hicho.

"Operesheni hii, ambayo ilikuwa ni sehemu ya ulinzi wa raia katika kanda hiyo, pia ilikua na lengo la kutoa msaada wa matibabu kwa watu wanaohitaji," alisema mkuu wa Minusma, Mahamat Saleh Annadif, akinukuliwa katika ripoti iliyolewa na Minusma, huku ikilaani shambulio hili jipya.

Ripoti hiyo imesifu "ujasiri" wa askari wa Minusma na jeshi la Mali "ambapo operesheni hiyo ya pamoja imesaidia kuangamiza magaidi kadhaa", huku ikitoa wito kuwa makini zaidi, mshikamano na umoja wa raia wa Mali kukabiliana na ujinga wa wapinzani wetu ", hapa ikimaanisha makundi ya kijihadi.