ZIMBABWE-SIASA-USALAMA

Rais mtarajiwa wa Zimbabwe kuapishwa Ijumaa hii

Emmerson Mnangagwa ataongoza Zimbabwe hadi kuelekea uchaguzi mkuu mwaka ujao.
Emmerson Mnangagwa ataongoza Zimbabwe hadi kuelekea uchaguzi mkuu mwaka ujao. REUTERS/Mike Hutchings

Rais mtarajiwa wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa anatarajiwa kutawazwa leo Ijumaa, siku tatu baada ya mtangulizi wake Robert Mugabe kuachia ngazi kwa shinikizo la jeshi na chama chake cha Zanu-PF.

Matangazo ya kibiashara

Aliyekua makamu wa rais anamrithi Mugabe, baada ya uhasama kati yake na mkewe Mugabe, Grace Mugabe, kutokea na kusababisha kufutwa kazi na kukimbilia nchini Afrika Kusini.

Grace Mugabe alitaka kumrithi mumewe, baada ya kukalia kiti cha makamu wa rais wa Zimbabwe.

Bw. Emmerson alirejea siku ya Jumatano jioni, siku moja tu baada ya mtangulizi wake kujiuzulu.

Kufutwa kwake kazi mwezi huu kulipelekea chama tawala cha Zanu-PF na jeshi kuingilia kati na kumlazimisha Mugabe ang'atuke .

Upinzani unamtaka Emmerson Mnangagwa, ambae amekuwa mmoja wa watawala kumaliza "utamaduni wa ufisadi".

Vyombo vya habari vya serikali vimesema kuwa Robert Mugabe atahudhuria sherehe za kuapishwa kwa Bw. Munangagwa.

Sherehe hizo zitafanyika katika uwanja wa michezo mjini Harare, huku waandalizi wakiwataka wa Zimbabwe kuhudhuria kwa wingi sherehe hizo.

Mugabe kapewa kinga

Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe amehakikishiwa usalama wake na familia yake na hatafunguliwa mashtaka yoyote baada ya kuondoka madarakani wiki hii.

Ripoti zinasema kuwa, hayo ni miongoni mwa mambo ambayo yalikubaliwa wakati wa mazungumzo ya kina kabla ya rais huyo wa zamani,mwenye umi wa miaka 93, aliyeongoza Zimbabwe kwa miaka 37, kukubali kuondoka.

Picha za kwanza zimekuwa zikisambaa katika mitandao ya kijamii, zikimwonesha Mugabe na mkewe Grace katika eneo ambalo halifahamiki, ikiwa ni picha za kwanza tangu kujiuzulu.

Usalama umeimarishwa nchini Zimabwe wakati huku Emmerson Mnangagwa akitarajiwa kutawazwa.

Emmerson Mnangagwa ataongoza Zimbabwe hadi kuelekea uchaguzi mkuu mwaka ujao.