MISRI-UGAIDI

Watu 235 wauawa nchini Misri baada ya kushambuliwa msikitini

Msikiti Kaskazini mwa Misri
Msikiti Kaskazini mwa Misri STRINGER / AFP

Watu 235 wamepoteza maisha katika mkoa wa Sinai nchini Misri baada ya watu waliokuwa wamejihami kwa silaha kuvamia na kushambulia Msikiti mmoja Kaskazini mwa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Hili ndilo shambulizi baya zaidi kuwahi kutokea na kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni.

Walioshuhudia shambulizi hili baya wanasema wavamizi hao wakiwa wamejihami kwa mabomu na silaha, walizingira msikiti huo na kuwashambulia waumini wa Kiislamu waliokuwa msikiti siku ya Ijumaa wakiwa ibadani.

Watu 109 wamejeruhiwa katika shambulizi hilo ambalo serikali ya Misri imesema ni la kigaidi.

Rais Abdel Fattah al-Sisi amelaani shambulizi hilo na kutangaza siku tatu za maombolezo kuwakumbuka waliopoteza maisha.

Al Sisi amesema serikali yake itatumia nguvu kulipiza kisasi dhidi ya magaidi hao.

Rais wa Marekani Donald Trump naye amelaani shambulizi hilo na kusema limetekelezwa na watu waoga.

Waziri wa Mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian na mwenzake wa Uingereza Boris Johnson nao pia wamelaani shambulizi hilo la kigaidi na kusema mataifa yao yanasimama na Misri.

Ahmed Abul Gheit, kiongozi wa muungano wa nchi za kiarabu lenye makao yake jijini Cairo, amesema wavamizi hao wamewauwa watu wasiokuwa na hatia.

Misri imeendelea kukabiliana na visa vya ugaidi nchini humo na kusababisha serikali kupiga makundi kama Muslim Brotherhood.