EU-AU-USHIRIKIANO

EU na AU wachukua hatua za kuzuia visa vya utumwa wa wahamiaji Libya

Wahamiaji 155 wa Cote d'Ivoire wakirudi kutoka Libya 20 Novemba 2017.
Wahamiaji 155 wa Cote d'Ivoire wakirudi kutoka Libya 20 Novemba 2017. ISSOUF SANOGO / AFP

Mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika unaendelea kwa siku ya pili mfululizo, huku suala la wahamiaji kuuzwa kama watumwa likigubika mkutano huo. Pia masuala ya ugaidi na ukosefu wa ajira kwa vijana yamekua yakizungumziwa katika mkutano huo.

Matangazo ya kibiashara

Viongozi kutoka mabara yote hayo mawili wanasema ni vema suala hilo la wahamiaji kuuzwa kama watumwa nchini Libya lishughulikiwe haraka iwezekanavyo. Siku ya Jumatano jioni viongozi tisa kati yao na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa walitoa hoja ya kuundwa kwa kikosi kitakacho ingilia kati ili kukomesha biashara ya wahamiaji nchini Libya na kuzuia raia wa Afrika kuendelea kukimbilia Ulaya. Kazi ya kwanza ya kikosi hiki ni kwenda kutafuta wahamiaji wanaozuiliwa nchini Libya ambao wanataka kurejea katika nchi zao.

Kwa jambo hili, Libya, kupitia Rais Fayez el-Sarraj, imekubali hoja hiyo ili "shughuli za kuwaondoa watu hao nchini Libya zifanyike siku zijazo au ndani ya wiki kadhaa".

Lakini ili kukabiliana na mitandao ya biashara ya binadamu, viongozi wanaoshiriki mkutano huo wameamua kuepo na mfumo wa kupeana taarifa na uchunguzi wa polisi ili kuvunja mitandao hiyo kwenye mipaka ya nchi husika. "Mitandao ya wahalifu, ambao wanajihusisha hasa na biashara ya silaha, dawa za kulevya na makundi ya kigaidi katika eneo la Sahel," alikumbusha rais wa Ufaransa Emmanuel Macron siku ya Jumatano usiku baada ya kikao cha kwanza cha mkutano huo kumalizika.

Pia wamekubaliana kuhamasisha vijana wa Kiafrika kupitia kampeni za mawasiliano kwa lengo la kuwazuia vijana kuelekea Ulaya, safari ambayo imekua ni ngumu kwao kutokana na madhila wanaopata katika safari hiyo.