DRC-MONUSCO-USALAMA

Monusco yataka kufanyika uchunguzi kuhusu kutumiwa kwa wapiganaji wa M23

Kundi la waasi wa zamani wa M23 katika kambi ya Bihanga, Februari 8, 2017.
Kundi la waasi wa zamani wa M23 katika kambi ya Bihanga, Februari 8, 2017. RFI/Gaël Grilhot

Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Monusco) inataka kufanyika uchunguzi kwa madai ya shirika la kimataifa la Haki za Binadam la Human Right Watch kuwa serikali ya DRC ilitumia wapiganaji wa zamani wa M23 kuwakabili waandamanaji.

Matangazo ya kibiashara

Mapema wiki hii shirika la kimataifa la haki za binadamu la Human Right Watch lilimtuhumu rais Joseph Kabila kuwasajili wapiganaji wa zamani wa kundi la M23 kwa lengo la kuwakandamiza waandamanaji waliokuwa wakipinga utawala wake Desemba 19 na 20 mwaka 2016 jijini Kinshasa.

Kwa mujibu wa shirika hilo, ukandamizaji ulisababisha vifo vya watu 60.

Serikali ya DR Congo kupitia waziri wake wa haki za binadamu Marie Ange Mushobeka, alisema ameshangazwa na ripoti hiyo na kwamba shirika hilo halina ushahidi wowote kuhusu tuhuma hizo.

Naye kiongozi wa zamani wa kundi la M23 Bertrand Bisimwa alisema serikali ya Congo imewaajiri kupitia mlango wa nyuma wapiganaji wa zamani walioasi kundi hilo waliofukuzwa.

Bw Bisimwa alisema wapiganaji walioonekana kusajiliwa na serikali ya Kinshasa ni wale waliokuwa wameondolewa katika kundi hilo muda mrefu.

Human Rughts Watch, iliisema uchunguzi wao umebaini ukweli huo baada ya kuzungumza na waasi hao wa zamani pamoja na familia zao.