SUDAN KUSINI-ETHIOPIA

Sudan Kusini: Mazungumzo ya amani kutamatika mjini Addis Ababa

Picha ya maktaba ikionesha wapiganaji wa waasi wakishangilia kwenye moja ya ushindi wao kwenye mji wa Upper Nile. February 13, 2014.
Picha ya maktaba ikionesha wapiganaji wa waasi wakishangilia kwenye moja ya ushindi wao kwenye mji wa Upper Nile. February 13, 2014. REUTERS/Goran Tomasevic/File Photo

Serikali ya Sudan Kusini na makundi ya waasi nchini humo wametiliana saini makubaliano ya kusitisha mapigano wakati wa mazungumzo ya amani yanayotarajiwa kutamatika Ijumaa hii jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Matangazo ya kibiashara

Makubaliano haya yamefikiwa ikiwa ni sehemu ya kujaribu kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo vilivyodumu kwa zaidi ya miaka minne.

Makubaliano yanasema pande zote zitatakiwa kusirisha mapigano kwenye maeneo waliyoko, kucha vitendo vyovyote ambavyo vitasababisha mapigano na kuwaachiliwa wafungwa wote wa kisiasa pamoja na wanawake na watoto waliotekwa.

Mwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika Moussa Faki amesema hatua iliyofikiwa ni ya awali na imetoa matumaini kwa wananchi ambao wanaendelea kutaabika kutokana na kuendelea kwa mapigano.

Viongozi wa Sudan Kusini kwa miongo kadhaa wamepigania uhuru wa taifa hilo lakini walipojitenga mwaka 211 kukaanza kushuhudiwa mvutano wa kimadaraka kati ya rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake wa rais Riek Machar na kusababisha kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013.

Mkataba wa amani ulitiwa saini miaka miwili baadae lakini ukavunjika mwezi Julai mwaka 2016 wakati mapigano mapya yalipoibuka mjini Juba na kusababisha makamu wa rais Machar kukimbia.

Upinzani uligawanyika huku Taban Deng akichukua nafasi ya makamu wa kwanza wa rais huku sehemu ya wanajeshi wa Machar wakirejea msituni kupigana.

Wakati mapigano ya awali yakielezwa kuwa ni kati ya kabila la Machar la Nuer na lile la rais Kiir Dinka, mapigano haya mapya yaliibua makundi mengine ya waasi.

Machafuko yalienea kusini mwa jimbo la Equatoria na kusababisha mamilioni ya rais wa Sudan Kusini kukimbilia kwenye nchi za Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuwa janga jingine kubwa la wakimbizi duniani.