DRC-UN-MONUSCO-USHIRIKIANO

Leila Zerrougui ateuliwa kuwa mkuu wa Monusco, DRC

Leila Zerrougui, kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa Monusco, alikuwa Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Watoto na Migogoro ya kivita.
Leila Zerrougui, kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa Monusco, alikuwa Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Watoto na Migogoro ya kivita. AFP/MOHAMMED HUWAIS

Leila Zerrougui, raia kutoka Algeria ameteuliwa kuchukua nafasi ya Maman Sidikou kama mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Monusco).

Matangazo ya kibiashara

Leila Zerrougui ataanza rasmi majukumu hayo Februari 1. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitangaza uteuzi huo siku ya Jumatano (Desemba 27).

Wagombea katika nafasi hiyo walikua wakikaribiana katika wiki za hivi karibuni. Abdoulaye Bathily, raia wa Senegal, ambaye alishindwa katika kinyang'anyiro cha kuwania uwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Mataifa mwaka jana, alikua miongoni mwa wagombea.

Alipambana katika kinyang'anyiro hicho na Leila Zerrougui, mwanadiplomasia wa Algeria mwenye umri wa miaka 61, mwanasheria, na ambaye pia maalumu katika masuala ya haki za binadamu. Wasifu wake umeonekana muhimu kwa majukumu ya kuiongoza Tume ya Umoja wa Mataifa nchini DRC.

Leila Zerrougui anafahamu vema DRC. Alikuwa Naibu Mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa nchini DRC kati ya mwaka 2008 na 2012 kabla ya kuteuliwa kuwa Mwakilishi Maalum kwa Watoto na Migogoro ya kivita kwenye Umoja wa Mataifa.

Lakini Bi Zrrougui atakua na kibaru kigumu, wakati huu nchi ya DRC inashuhudia mdodroro wa usalama na mvutano wa kisiasa unaoendelea. Mtangulizi wake alikosolewa mara kadhaa, hasa wakati wa mgogoro wa Kasai. Maman Sidikou anatolewa kwenye nafasi hiyo siku chache baada ya kikosi cha Umoja wa Mataifa, Monusco kupoteza askari wake 15 kutoka Tanzania waliouawa katika kambi yao katika mazingira ambayo ya kutatanisha.

Leila Zerrougui ataanza rasmi majukumu yake miezi miwili kabla ya Tume ya Umoja wa Mataifa (Monusco) kuongezewa muda wa majukumu yake nchini DRC. Monusco tayari imepunguziwa bajeti yake ya matumizi wakati ambapo hali ya usalama inaendelea kudororo kila kukicha.