LIBERIA

Liberia: George Weah achaguliwa kuwa rais wa Liberia kwa kishindo

Rais mpya wa Liberia George Weah.
Rais mpya wa Liberia George Weah. REUTERS/Thierry Gouegnon

Mwanasoka wa zamani wa Liberia George Weah amechaguliwa kuwa rais mteule ikiwa ni katika jaribio lake la pili toka awanie urais wa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Wakati huu ambapo karibu kura zote zimeshahesabiwa katika uchaguzi wa duru ya pili, Weah anaongoza kwa kumuacha mbali mpinzani wake na makamu wa rais Joseph Boakai.

Weah atachukua nafasi ya Ellen Johnson Sirleaf ambaye alikuwa rais wa kwanza mwanamke barani Afrika kuchaguliwa kidemokrasia na sasa anatarajiwa kukabidhi madaraka kwa amani.

Rais Sirleaf alimshinda Weah katika uchaguzi wa duru ya pili uliofanyika mwaka 2005, baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miongo kadhaa nchini humo.

Punde baada ya taarifa za ushindi wa Weah kuanza kuenea, maelfu ya wafuasi wake wamejitokeza kwenye viunga vya miji mbalimbali nchini humo kushangilia ushindi wake, mamia ya watu wameonekana mjini Monrovia wakishangilia.

Mwanasoka huyu wa zamani aliyefanya kampeni zake chini ya muungano wa mabadiliko ya kidemokrasia, aliwashawishi vijana kumpigia kura huku mpinzani wake makamu wa rais Boakai akionekana kama mzee.

Hata hivyo ushindi wa Weah umekuja huku akikabiliwa na ukosolewaji kutokana na kumteua mgombea mwenza wake Jewel Taylor aliyekuwa mke wa rais wa zamani wa nchi hiyo Charles Taylor anayetumikia kifungo nchini Uingereza kwa makosa ya kivita.

Weah mwenye umri wa miaka 51 alishinda duru ya kwanza ya uchaguzi huu uliofanyika mwezi Octoba kwa asilimia 38.4 ukilinganisha na mpinzani wake aliyepata asilimia 28.8, matokeo ambayo yaliwafanya wagombea wote wawili kwenda kwenye duru ya pili.

Tume ya taifa ya uchaguzi nchini Liberia siku ya Alhamisi ilisema kuwa zaidi ya asilimia 98.1 ya kura zote zimeshahesabiwa na Weah alikuwa anaongoza kwa asilimia 61.5 huku mpinzani wake Boakai akiwa na asilimia 38.5.

Weah amewahi kuvichezea soka vilabu kadhaa barani Ulaya ikiwemo klabu ya AC Milan ya Italia, Chelsea ya Uingereza na PSG ya Ufarana, na amekuwa mchezaji pekee kutoka barani Afrika kushinda taji la mchezaji bora wa dunia inayotolewa na shirikisho la mpira duniani Fifa.

Mwanasoka huyu aliingia kwenye siasa mwaka 2002 baada ya kustaafu soka na kwa sasa alikuwa seneta katika bunge la Liberia.

Nchi ya Liberia iliyojengwa na watumwa weusi wa Kimarekani katika karne ya 19, haijawahi kuwa na mabadilishano ya madaraka ya amani kutoka kwa rais mmoja kwenda mwingine tangu mwaka 1944.

Pingamizi la kisheria lilichelewesha uchaguzi huu wa duru ya pili kwa majuma saba na idadi ya watu waliojitokeza kuoiga kura ilikuwa ndogo ukilinganisha na iole iliyojitokeza kwenye uchaguzi wa mwezi Octoba.

Zaidi ya watu milioni 2 walikuwa wamesajiliwa kupiga kura katika taifa hilo lenye watu milioni 4.6.

Rais Sirleaf alichukua madaraka mwaka 2006 baada ya mtangulizi wake Charles Taylor kulazimishwa kuondoka madarakani na waasi mwaka 2003 na kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Taylor anahudumu kifungo chake cha miaka 50 jela nchini Uingereza kwa makosa ya uhalifu wa kivita kwenye mzozo wa nchi jirani ya Sierra Leone.