DRC-UN-USALAMA

Umoja wa Mataifa wataka kufanyike uchunguzi baada ya machafuko ya Desemba 31 DRC

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anaehusika na masuala ya amani, Jean-Pierre Lacroix, ameomba uchunguzi ufanyike kuhusu wahusika wa machafuko ya tarehe 31 Desemba yaliyotekelezwa na vikosi vya usalama vya DRC dhidi ya raia.

Viongozi wa kanisa Katoliki nchini DRC katika maandamano dhidi ya seriklai Januari 1, 2018 Kinshasa, DRC.
Viongozi wa kanisa Katoliki nchini DRC katika maandamano dhidi ya seriklai Januari 1, 2018 Kinshasa, DRC. John WESSELS / AFP
Matangazo ya kibiashara

Umoja wa Mataifa unaomba ufanyike uchunguzi kuhusu wahusika wa machafuko, "amesema Jean-Pierre Lacroix mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na kubaini kwamba kazi ya walinda amani " ilivurugwa" siku hiyo na vikosi vya usalama vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa na Kanisa Katoliki nchini DRC, watu wasiopungua watano waliuawa wakati plisi ilikua ikitawanya maandamano yaliyoitishwa tarehe 31 Desemba na viongozi wa kanisa Katoliki nchini humo, ambao walimuomba Rais Joseph Kabila kutangaza hadharani kwamba atajiuzulu na hatowania katika uchaguzi ujao.

Rais Joseph Kabila hajaandaa uchaguzi katika nchi yake wakati ambapo muhula wake wa pili na wa mwisho ulimalizika tarehe 20 Desemba, na kusababisha maandamano mabaya mnamo mwezi Septemba na Desemba mwaka uliopita. Uchaguzi unaoandaa kuondoka kwake na kumtafuta mrithi wake yamepangwa kufanyika Desemba 23, 2018.

Kwa mujibu wa kanisa Katoliki, parukia 134 zilizingirwa na misa tano zilisitishwa tarehe 31 Desemba.

"Hali ya kisiasa bado ni tete" na "hali ya usalama ni ya wasiwasi," amesema Jean-Pierre Lacroix. "Mazungumzo ndio njia pekee" ili kuondokana katika mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini DRC, ameongeza, huku akitoa wito wa tahadhari kabla ya kitendo chochote ambacho kinaweza kusababisha vurugu na kuonya dhidi ucheleweshaji zaidi wa kalenda ya uchaguzi.

Balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa, François Delattre, "ameshutumu vurugu" zilizosababishwa na vikosi vya usalama.

Mwanzoni mwa mwezi Januari, serikali "ilishukuru vikosi vya usalama ambavyo, nchini kote, viliheshimu agizo vilivyopewa, kulingana na sheria ya kimataifa ya kibinadamu katika kudhibiti" maandamano ya Desemba 31, 2017.

Lacroix sasa anataka mamlaka nchini DRC kuanzisha uchunguzi maalumu kubaini waliohusika na uvamizi wa kwenye makanisa na kuwafungulia mashtaka kwa ukiukaji wa haki za binadamu.