Video mpya ya Boko Haram yaonesha wasichana wa Chibok

Kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Boko Haram limerusha leo Jumatatu video mpya inayoonyesha wanafunzi wasichana 14 waliotekwa katika mji wa Chibok, kaskazini mwa Nigeria, mnamo mwezi Aprili 2014.

Baadhi ya wasichana waliotekwa na Boko Haram katika mji wa Chibok, Nigeria.
Baadhi ya wasichana waliotekwa na Boko Haram katika mji wa Chibok, Nigeria. © Reuters
Matangazo ya kibiashara

"Sisi ni wasichana wa chibok (...) Kwa uwezo wake Mungu, hatutorudi," msichana mmoja amesema kwa niaba ya kundi la wasichana hao walionekana kwenye mkanda wa video ya muda wa dakika 21, ikiwa ni pamoja na wasichana watatu wakishikilia mikononi watoto wachanga.

Hii ni video ya kwanza ya aina hii tangu mwezi Mei, wakati msichana mmoja alisema yeye ni miongoni mwa wanaunzi wasichana 219 waliotekwa katika mji wa Chibok, alionekana akishikilia bunduki na yeye pia alikataa kurudi nyumbani.

Hakuna kitu kinachoonyesha wakati na mahali video hiyo ilirekodiwa, wala kuonyesha kuwa wasichana hao wamelazimishwa kufanya hivyo.

"Sisi tunawasikitikia wasichana wengine wa Chibok ambao waliamua kurudi nchini Nigeria. Mungu aliwabariki na kuwapeleka kwa Khalifa (sehemu takatifu) lakini badala yake, muliamua kurudi katika uovu ", ameendelea msichana huyo akiwaonya wasichana waliofanikiwa kutoroka kundi hilo wakati walipotekwa nyara karibu miaka nne iliyopita.

Msichana huyo pia amewaambia wazazi wake: "mnapaswa kutubu (...) moto wa Jahannamu nimakazi yenu ikiwa hamtotubu, kwa sababu Allah ametuumba ili tumuabudu".

Pia amemshukuru kiongozi wa kundi la Boko Haram, "baba yetu Abubakar Shekau, ambaye alituoa, tunaishi katika faraja (...) Abubakar Shekau ni kiongozi wetu".

Shekau ambaye alidaiwa mara kadhaa kuwa alifariki, pia ameonekana kwenye video hiyo, akirusha risasi kwa bunduki kubwa ya kivita kabla ya kutoa mahubiri yanayodumu dakika 13.

Jumla ya wasichana 276 walikamatwa mnamo mwezi Aprili 2014 katika shule yao ya sekondari huko Chibok, katika jimbo la Borno, na kusababisha manung'uniko kimataifa.