DRC-SIASA-MAANDAMANO-CENCO

Waandamanaji sita wapoteza maisha katika makabiliano na polisi nchini DRC

Maandamano dhidi ya rais Joseph Kabila Januari 21 2018
Maandamano dhidi ya rais Joseph Kabila Januari 21 2018 © REUTERS / Kenny Katombe

Hali ya wasiwasi imeendelea kushuhudiwa jijini Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo licha ya utulivu kuanza kushuhudiwa katika jiji hilo baada ya makabiliano makali kati ya waandamanaji na maafisa wa usalama.

Matangazo ya kibiashara

Umoja wa Mataifa umesema watu sita wamepoteza maisha  wakati polisi nchini humo wakisema watu wawili ndio walipoteza maisha.

Nao waharakati wameeleza kuwa watu 247 wametiwa nguvuni, wakati watu 23 wakijeruhiwa kwa kupigwa risasi.

Mwanasiasa wa upinzani Vital Kamerhe amesema kabla ya maandamano hayo, waandamanaji walikuwa wamenuia kupambana na maafisa wa polisi.

Msemaji wa jeshi la kulinda amani nchini humo MONUSCO Florence Marshal amesema amesikitishwa na kile kilichoshuhudiwa wakati wa maandamano hayo.

Makumi ya watu pia walijeruhiwa na kukamatwa katika miji ya Mashariki hasa Goma, Bukavu na Butembo.

Kanisa Katoliki, limesema kuwa maandamano hayo yataendelea katika siku zijazo, kuendelea kushinikiza kuondoka madarakani kwa rais Joseph Kabila.