DRC, KANISA-MAANDAMANO-USALAMA

Kadinali Monsengwo alaani ghasia dhidi ya waandamanaji DRC

Kadinali Laurent Monsengwo katikati kwenye picha.
Kadinali Laurent Monsengwo katikati kwenye picha. CC/Carolus

Askofu mkuu wa kanisa Katoliki jijini Kinshasa, Kadinali Laurent Monsengwo ametoa wito kwa viongozi wa serikali nchini humo kujitafakari kuhusu matukio ya ghasia dhidi ya waandamanaji yaliyotokea Jumapili iliyopita.

Matangazo ya kibiashara

Kadinali Monsengwo amelani mauaji ya waandamanaji ambayo Umoja wa Mataifa nchini jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo Monusco inasema watu 6 ndio walipoteza maisha, wakati polisi ikisisitiza kwamba ni watu 2.

Hata hivyo Kadinali Monsengwo amewataka waumini wa kanisa katoliki kuendelea kushikamana.

Hayo yanajiri wakati ambapo Padri Robert Masinda alitekwa jana Jumanne karibu na mji wa Beni na kundi la watu wasiojulikana wakati akitoka shambani pamoja na kundi la watu wengine wanne wakiwemo wahandisi wawili. Hili ni tukio la nne katika kipindi cha miezi sita.

Mashirika ya kiraia mjini Beni yamewatolea wito viongozi wa serikali na kikosi cha Monusco kufanya kila jitihada kuwapata mateka hao.

Katika hatua nyingine wafuasi 11 wa Lucha waliokuwa wametiwa nguvuni katika mji wa Kananga katikati mwa nchi wameachiwa huru baada ya kutuhumiwa kuendesha vurugu na kutotii amri ya viongozi wa serikali.

Wakati huo huo mtandao umerejeshwa tena chini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, baada ya kufungwa Jumamosi iliyopita, kuelekea siku ya maandamano dhidi ya rais Joseph Kabila Jumapili iliyopita.

Raia wa DRC toka siku ya Jumamosi wamekuwa wakishindwa kutumia mitandao ya kijamii lakini pia imekuwa vigumu kutuma ujumbe mfupi kupitia simu za mkononi.

Serikali ya DRC katika siku za hivi karibuni, imekuwa ikiagiza kampuni za simu kufunga mtandao kuelekea maandamano yanayopangwa na Kanisa Katoliki kwa hofu kuwa uwepo wa mtandao unaweza kuchochea zaidi maandamano hayo.