Uhusiano wa kidiplomasia wadorora kati ya DRC na Ubelgiji

Serikali ya DRC imechukua hatua ya kusitisha shughuli za shirika la Ubelgiji la maendeleo (Enabel) katika nchi yake kufuatia Ubelgiji kutangaza nia yake ya kusitisha misaada kwa serikali ya DRC kutokana na hali ya kisiasa na kibinadamu inayoendelea DRC.
Serikali ya DRC imechukua hatua ya kusitisha shughuli za shirika la Ubelgiji la maendeleo (Enabel) katika nchi yake kufuatia Ubelgiji kutangaza nia yake ya kusitisha misaada kwa serikali ya DRC kutokana na hali ya kisiasa na kibinadamu inayoendelea DRC. REUTERS/Yves Herman/File Photo

Barua iliyovujishwa kwa vyombo vya habari nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, inaonesha kuwa, kuna mpango wa serikali ya Kinshasa kufunga Ubalozi wa Ubelgiji nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii inaonesha uhusiano mbaya wa kidiplomasia kati ya DRC na Ubelgiji ambao ndio walikuwa wakoloni wa taifa hilo la Afrika ya Kati.

Ubelgiji inasema kuwa inasikitishwa na tangazo la serikali ya DRC kusitisha shughuli za shirika la Ubelgiji la maendeleo (Enabel) katika nchi yake, lakini pia kufuta taasisi ya Schengen, taasisi ambayo inaruhusu raia wa DRC kupata visa za nchi 17 kati ya nchi za Umoja wa Ulaya. Uamuzi huu ni ulipizaji kisasi, kufuatia Ubelgiji kutangaza nia yake ya kusitisha misaada kwa serikali ya DRC kutokana na hali ya kisiasa na kibinadamu inayoendelea DRC.

Ubelgiji na mataifa ya Umoja wa Ulaya yamekuwa yakiistumu serikali ya rais Joseph Kabila kwa kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji wanaomtaka aondoke madarakani.

Hivi karibuni Ubelgiji ilitangaza kusitisha msaada wa kifedha kwa DRC kwa sababu ya hali ya kisiasa nchini humo.

Serikali ya Kinshasa imeendelea kushtumiwa makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na uvunjaji wa hki za binadamu, kuminya uhuru wa kujieleza, huru wa kuandamana na mikutano pamoja na kuwakandamiza wapinzani.

Hata hivyo serikali ya DRC imekanusha shutma hizo dhidi yake na kusema kuwa ni uzushi usio kuwa na msingi.