DRC-KABILA-SIASA-UCHAGUZI

Rais Kabila asema anaheshimu Kalenda ya Uchaguzi

Rais wa DRC  Joseph Kabila.
Rais wa DRC Joseph Kabila. REUTERS/Kenny Katombe/File Photo

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila, amesema anaheshimu ratiba ya Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Kabila ambaye amekuwa akiongoza nchi hiyo tangu mwaka 2001, akizungumza jijini Kinshasa, hata hivyo hajasema iwapo atawania tena wadhifa huo.

“Tutakuwa na Uchaguzi kama ulivyopangwa,” alisema rais Kabila.

“Naona upande ule mwingine, hauna mpango wowote, sisi tuna mpango,” aliongeza.

Aidha, amekanusha madai ya vikosi vya usalama kutumia nguvu kupita kiasi kusambaratisha maandamano ya amani, yanayomtaka aondoke madarakani.

Kanisa Katoliki ambalo lilifanikiwa kuja na mwafaka wa kisiasa mwaka 2016, ambao haujatekelezwa, limekuwa likiandaa maandamano hayo na limesema litaendelea kumshinikiza Kabila kuondoka.

Maandamano ya wiki iliyopita, yalisababisha vifio vya watu sita kwa mujibu wa takwimu za umoja wa Mataifa baada ya makabiliano kati ya waandamanaji na polisi.