KENYA-SIASA-UCHAGUZI

NASA kumwapisha Odinga huku Polisi ikisema haitakubali mkutano Uhuru Park

Raila Odinga, kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya NASA
Raila Odinga, kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya NASA REUTERS/Baz Ratner

Muungano wa upinzani nchini Kenya NASA, unasema maandalizi yamekamilika kuelekea kumwapisha kiongozi wake Raila Odinga kama rais watu siku ya Jumanne katika bustani ya uhuru jijini Nairobi.

Matangazo ya kibiashara

Mkurugenzi Mkuu wa NASA Norman Magaya amewaambia wafuasi wa NASA kuwasili katika bustani hiyo kufikia saa mbili asubuhi kwa maandalizi ya kumwapisha Odinga na Naibu wake Kalonzo Musyoka saa nne asubuhi.

Licha ya hakikisho hilo, wasiwasi umezuka kuhusu iwapo shughuli hiyo itafanyika katika bustani hiyo baada ya jeshi la Polisi kupiga marufuku mkusanyiko wa watu katika bustani hiyo.

Kabla ya Polisi kupiga marufuku hayo, serikali ya Kaunti ya Nairobi kufunga bustani hiyo kwa ukarabati.

Kamanda wa jiji la Nairobi Japhet Koome, amesema hataruhusu yeyote kuonekana katika bustani hiyo.

“Siwezi kuruhusu watu kwenda kuumizana katika bustani ya Uhuru Park,” alisema.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, viongozi wa NASA walisema shughuli za kumwapisha Odnga lazima zifanyike baada ya kumtuhumu rais Kenyatta kukataa mazungumzo ya kisiasa baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka uliopita.

Kiongozi wa Kanisa Angilikana nchini humo Jackson Olesapit ametaka Odinga kuruhusiwa kuendelea na shughuli hiyo kwa amani, ili kuepuka makabiliano kati ya polisi na wafuasi wa NASA.

Kenyatta amekuwa akisema kuwa, mazungumzo pekee anayotaka ni yale yanayolenga kuleta maendeleo nchini humo.