DRC-USALAMA

John Tshibangu azuiliwa kusikojulikana DRC

Kanali John Tshibangu aliasi na kutangaza vita dhidi ya Rais Kabila, huku akiimpa siku 45 aachie madaraka.
Kanali John Tshibangu aliasi na kutangaza vita dhidi ya Rais Kabila, huku akiimpa siku 45 aachie madaraka. REUTERS/Kenny Katombe

John Tshibangu, Kanali muasi, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, amefikishwa nchini humo na kuzuiliwa kusikojulikana nchini humo, baada ya kukamatwa nchini Tanzania.

Matangazo ya kibiashara

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasa ya Kongo imethibitisha kumpokea Kanali John Tshibangu aliyekamatwa na vyombo vya usalama vya Tanzania juma moja lililopita baada ya kuonekana kwenye mkanda wa video akimpa siku 45 rais Joseph Kabila awe amejiuzulu au aipindue Serikali yake.

Waziri wa Sheria nchini DRC Alexis Tambwe Mwamba amethibitisha kusafirishwa nchini humo kwa kanali Tshibangu na kusisitiza kuwa kesi yake itasikilizwa kwa uwazi kama zilivyo kesi nyingine akithibitisha kuwa atashtakiwa kwa makosa ya uhaini.

Mke wa kanali Tshibangu, Mokee Tshibangu akiongea na idhaa ya Kiswahili ya RFI, amesema anahofia maisha ya mume wake na kuiomba Serikali isimchukulie mume wake kama muasi bali kama kamanda aliyeasi jeshi.

Rais Kabila alimaliza muhula wake wa pili na wa mwisho kikatiba kuwa Rais mwezi Disemba 2016 lakini hajaachia madaraka, mengi yamesemwa na Serikali ikiwemo “hatuna pesa za kutosha kufanya Uchaguzi Mkuu”.

January 19, 2018 Kanali John Tshibangu aliasi na kutangaza vita dhidi ya Rais Kabila, huku akiimpa siku 45 aachie madaraka.

Asubuhi ya Ijumaa January 19 2018 Wanajeshi walionekana kuizingira kwa wingi Ikulu ya Kinshasa, huku video iliyorekodiwa na Kanali Tshibangu ikiendelea kusambaa ambapo ndani yake alionekana kazingirwa na Wanajeshi wenye silaha.

Kwenye video hiyo Tshibangu alinukuliwa akisema “Nafahamu siri ya Rais Kabila, sasa ni muda wa kuondoa Serikali ya Mabeberu na Udikteta, na ni lazima Rais Kabila aombe msamaha kwa Wakongo kuanzia Makanisani, Shuleni na hata Raia wa kawaida kwa kosa la kushindwa kuiongoza nchi”.

“Mimi kama Mwananchi mwenye msimamo na huruma kwa mateso yenu, niliamua kujitokeza ili kumfukuza Joseph Kabila kwa nguvu za vita na kijeshi, nawahakikishia kwamba tutamuwinda na atakimbia, ” alisema John Tshibangu.

Tshibangu alilitaja kundi lake la Waasi kwamba linaitwa “Forces Nouvelles du Congo” ikimaanisha Nguvu Mpya kwa Ajili ya Congo.

Rais Kabila anaendelea kukabiliwa na upinzani mkali kutokana na nia yake ya kutaka kugombea Urais kwa muhula wa tatu baada ya muhula wake wapili kumalizika mwezi Disemba 2016.