LIBERIA-MAREKANI-HAKI

Waathirika wa mauaji ya Liberia wawasilisha mashitaka katika mahakama ya Marekani

Mnamo Julai 2003, maelfu ya Waliberia walikimbia maeneo ya mapigano. Baadhi yao walikimbilia nchini Marekani.
Mnamo Julai 2003, maelfu ya Waliberia walikimbia maeneo ya mapigano. Baadhi yao walikimbilia nchini Marekani. AFP/Georges Gobet

Watu wanne walionusurika katika mauaji yaliyotokea katika kanisa nchini Liberia wamewasilisha mashitaka katika mahakama ya Marekani dhidi ya mtu anayeshtumiwa kuongoza mauaji hayo.

Matangazo ya kibiashara

Watu 600 waliuawa mwezi Julai 1990 wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Mashitaka yaliyowasilishwa katika mahakama ya Philadelphia, yanamshtumu Moses Thomas, afisa wa jeshi, alieongoza kikosi cha jeshi cha kupambana na ugaidi, kuamuru askari wake kutekeleza mauaji hayo.

Moses Thomas aliingia nchini Marekani katika sehemu ya programu ya uhamiaji kwa kusaidia waathirika wa vita. Kwa sasa anaishi katika kitongoji cha Philadelphia, imeandikwa kwenye mashitaka hayo.

Mashtaka hayo "yanashangaza," Moses Thomas aliiambia BBC, kulingana na habari iliyochapishwa kwenye tovuti ya redio na televisheni ya umma ya Uingereza.

Mauaji ya Julai 29, 1990 yalikua ni moja ya maovu makubwa zaidi yaliyofanyika dhidi raia wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka 14 nchini Liberia,na kuendelea hadi mwishoni mwa mwaka 2003.

Mnamo Julai 29, familia kadhaa zilizokimbia vurugu katika mji wa Monrovia, mji mkuu wa Liberia, zilikimbilia katika Kanisa ya St Peter Lutheran, ambapo kulikua kumejegwa kituo cha mapokezi cha shirika la Msalaba Mwekundu.

Kulingana na mashitaka, Moses Thomas aliwaagiza askari 45 kuingia kanisani na kufyatulia watu risasi bila kujali. Askari pia walitumia mapanga kwa kuwamalizia wale ambao walikua bado hawajafariki. Watu wengine walinusurikabaada ya kujificha chini ya maiti.

Ikiwa mashitaka hayo yatapokelewa, walalamikaji watapata tu fidia ya fedha. Wanasheria wa waathirika wanasema kwamba hakujawahi kamwe kuepo kwa mahakama ya kuchunguza uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanywa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Liberia.