DRC-RWANDA-USALAMA

Mapigano makali kati ya jeshi la DRC na jeshi la Rwanda

Askari wa DRC wakipiga doria katika hifadhi ya wanyama ya Virunga katika eneo la Mikeno.
Askari wa DRC wakipiga doria katika hifadhi ya wanyama ya Virunga katika eneo la Mikeno. RFI/Léa-Lisa Westerhoff

Mapigano makali kati ya jeshi la DRC na lile la Rwanda yalitokea siku ya Jumanne, Februari 13 mchana katika eneo la Bikenge, katika mbuga ya wanyama ya Virunga, kwenye Mlima wa Visoke.

Matangazo ya kibiashara

DRC inashutumu jeshi la Rwanda kuingia katika aridhi yake na tayari limewasilisha madai yake kwa kamati ya mseto ya uchunguzi ya Jumuiya ya nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) kwa ajili ya uchunguzi. Inaarifiwa kuwa pande zote mbili zilipoteza askari wake katika mapigano hayo.

Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la DRC katika eneo hilo, hali hiyo ilianza kujitokeza karibu wiki moja iliyopita ambapo watu wasiojulikana walionekana kwenye mpaka, upande wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kutokana na hali hiyo, serikali ya DRC iliwatuma askari wake siku ya Jumanne katika eneo hilo ili kupata taarifa zaidi.

Wakati jeshi letu lilikua likipiga doria lilishambuliwa kwa risasi. Baada ya ufyatulianaji risasi adua alionekana kuwa ni askari wa Rwanda, "amesema Guillaume Ndjike-Kaiko.

Kwa upande wa DRC, wanasema kuwa wana uhakika kuwa jeshi la Rwanda limeingia katika ardhi yao. Lakini vitu vinavyoonyesha mipaka kati ya nchi hizo havijawekwa.

Wakati huo huo serikali ya DRC iliwasilisha madai yao kwa tume inayohusika na masuala ya mipaka. "Ushahidi tunao ni kwamba jeshi la Rwanda lilikua likipiga kambi katika eneo letu, mita 200 hadi 400 kwa urefu. Hata hivyo, tumeomba tume ya mseto kuchunguza madai yetu. Ni baada ya uthibitisho huo tutaweza kupata ufumbuzi wa uhakika, "Valérien Mbalutwirandi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Mkoa wa Kivu Kaskazini.

Tume ya mseto tayari umetuma timu yake upande wa Rwanda mapema Jumatano jioni na ina matumaini ya kumaliza kazi yake ndani ya wiki moja. Hakuna taarifa rasmi kutoka upande wa Rwanda.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP inaonekana kuwa ni tatizo la ugawaji wa mipaka ndio chanzo cha mgogoro huo.