DRC-USALAMA-SIASA

Makazi ya Rais Kabila yashambuliwa Kabasha

Rais Kabila aendelea kushinikizwa kutowania muhula mwengine.
Rais Kabila aendelea kushinikizwa kutowania muhula mwengine. REUTERS/Kenny Katombe/File Photo

Waasi wa kundi la Mai-Mai mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameshambulia makaazi binafsi ya rais Joseph Kabila katika eneo la Kabasha.

Matangazo ya kibiashara

Shambulio hilo lilithibitishwa na msemaji wa jeshi la Congo ambae hata hivyo alijizuia kutoa takwimu za waliojeruhiwa au kupoteza maisha wakati wa mapigano.

Mashirika ya kiraia nchini DR Congo yanasema watu 3 wamepoteza maisha ambao ni waasi, huku jeshi likisadikiwa kuwateka waasi kadhaa.

Mashuhuda kutoka katika eneo la tukio wamesema mapema jana asubuhi waasi wanaoshukiwa kuwa Mai-Mai Mazembe walijitokeza katika eneo la Kabasha katika barabara itokayo Beni kuelekea Butembo mkoa wa kivu kaskazini, wakati wakijaribu kuvamia shamba binafsi la Rais Kabla ndipo wakakutana na moto wa wanajeshi walinzi wa kikosi cha ulinzi wa taasisi za serikali.

Mapigano hayo yalisababisha wananchi wa eneo la Kabasha kutoroka makwao wakati wapiganaji hao wakidhibitiwa na jeshi.

Shambulio jingine kama hilo dhidi ya maeneo yanayomilikiwa na rais Joseph Kabila lilitokea wakati wa siku kuu ya Krismasi huko Musenene Kivu ya Kaskazini.