DRC-MAANDAMANO

Wakaazi wa Bukavu waandamana kulalamikia utovu wa usalama

Mji wa Bukavu Mashariki mwa DRC
Mji wa Bukavu Mashariki mwa DRC www.rfi.fr

Wakaazi wa mji wa Bukavu Mashariki wa DRC waliandamana siku ya Ijumaa kuonesha gadhabu zao  kutokana na utovu wa usalama baada ya watu watatu kupatikana wameuwa siku ya Alhamisi.

Matangazo ya kibiashara

Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kujaribu kuwasambaratisha waandamanaji hao waliokuwa na hasira kutokana na kile ambacho Mashirika ya kiraia yanasema ni ongezeko la mauaji ya raia katika mji huo.

Aidha, Mashirika hayo ya kiraia yanasema tangu kuanza kwa mwaka huu, watu zaidi ya 30 wamepoteza maisha katika mji huo kwa sababu ya utovu wa usalama.

Waandamanaji walibeba mwili wa mmoja wa watu aliyekuwa ameuawa hadi katika bunge la mkoa, kuonesha kutofurahishwa na kile ambacho wanasema viongozi hao hawafanyi vya kutosha kukabiliana na utovu wa usalama.

Hii ndio mara ya kwanza kushuhudiwa kwa maandamano makubwa kama haya, yaliyodumu kwa saa kadhaa na kutatiza shughuli za kibiashara na usafiri baada ya waandamanaji kufunga barabara.

Ukosefu wa usalama ni suala linaloendelea kuwakabili wakaazi wa Mashariki mwa DRC kutokana na uwepo wa makundi mengi ya waasi.