DRC-SIASA-MAANDAMANO-CENCO

Mtu mmoja auawa jijini Kinsasha wakati wa maandamano dhidi ya rais Kabila

Polisi wa kupambana na ghasia jijini Kinshasa akiwa katika Kanisa Katoliki  Notre-Dame  tayari kukabiliana na waandamanaji Februari 25 2018
Polisi wa kupambana na ghasia jijini Kinshasa akiwa katika Kanisa Katoliki Notre-Dame tayari kukabiliana na waandamanaji Februari 25 2018 REUTERS/Goran Tomasevic

Mtu mmoja ameuawa jijini Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na wengine wanne kujeruhiwa wakati wa maandamano ya kumshinikiza rais Joseph Kabila kujiuzulu.

Matangazo ya kibiashara

Maandamano ya leo yamekuwa ya tatu mwaka huu yakiandaliwa na Kanisa Katoliki nchini humo kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Desemba.

Mamia ya waandamanaji walionekana katika jiji la Kinshasa na miji mingine wakiandamana licha ya serikali kuyapiga marufuku maandamano haya.

Idadi kubwa ya waandamanaji hao waliokuwa wametokea Kanisani,walitawanywa na maafisa wa Polisi waliokuwa wamejihami.

Mjini Kinsangani Kaskazini mwa nchi hiyo, hali ilikuwa hiyo, huku watu wawili wakijeruhiwa baada ya kupigwa risasi na Polisi.

Makasisi matatu wamekamatwa baada ya kuongoza maandamano hayo kwa mujibu wa ripota wa AFP.

Maandamano yaliyopita, yalisababisha vifo vya watu 15, wengi wakiwa wakaazi wa jiji kuu Kinshasa.

Serikali kwa mara nyingine, imefunga mtandao ili kuzuia mawasiliano kupitia mitandao ya kijamii lakini pia kuzuia watu kuwasiliana kwa ujumbe mfupi wa simu.

Kanisa Katoliki nchini humo limesema, litaendelea kuandaa maandamano haya hadi pale rais Kabila ambaye alianza kuongoza nchi hiyo mwaka 2001 atakapoondoka madarakani.

Kuna wasiwasi kuwa, Kabila ambaye muda wake wa kukaa madarakani ulimalizika mwaka 2016, anaweza kuwania tena wakati wa Uchaguzi Mkuu mwezi Desemba.