DRC.MAANDAMANo USALAMA

Watu 2 wauawa katika maandamano DRC

Kinshasa, Februari 26, 2018. Vifo vya watu wawili vimeorodheshwa na vyombo vya habari na Umoja wa Mataifa wakati wa ukandamizaji wa maandamano mapya yaliyoandaliwa na kanisa Katoliki.
Kinshasa, Februari 26, 2018. Vifo vya watu wawili vimeorodheshwa na vyombo vya habari na Umoja wa Mataifa wakati wa ukandamizaji wa maandamano mapya yaliyoandaliwa na kanisa Katoliki. John WESSELS / AFP

Watu wawili waliuawa nchini DRC jana Jumapili Februari 25 katika ukandamizaji dhidi ya maandamano yaliyoandaliwa na kanisa Katoliki dhidi ya Rais Kabila.

Matangazo ya kibiashara

Mtu mmoja alipigwa risasi na kufariki pao hapo mjini Kinshasa na mwingine alifariki kutokana na majeraha alioyapata Mbadanka, kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa, ambayo pia iliripoti kuwa watu 47 walijeruhiwa na zaidi ya 100 kukamatwa nchini kote.

Katika hotuba yake kwenye runinga ya taifa RTNC, msemaji wa polisi alihakikisha kuwa hakuna mtu yeyote aliyepoteza maisha, ispokua tu watu wawili waliojeruhiwa ambao walikuwa wahalifu na baadhi ya watu walikamatwa katika mji wa Goma. Hata hivyo tume ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Monusco) inaomba kufanyika uchunguzi.

Maandamano ya hayo yalikuwa ya tatu mwaka huu yakiandaliwa na Kanisa Katoliki nchini humo kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Desemba.

Mamia ya waandamanaji walionekana katika jiji la Kinshasa na miji mingine wakiandamana licha ya serikali kuyapiga marufuku maandamano.

Idadi kubwa ya waandamanaji hao waliokuwa wametokea Kanisani,walitawanywa na maafisa wa Polisi waliokuwa wamejihami.

Mjini Kinsangani Kaskazini mwa nchi hiyo, hali ilikuwa hiyo, huku watu wawili wakijeruhiwa baada ya kupigwa risasi na Polisi.

Makasisi watatu wamekamatwa baada ya kuongoza maandamano hayo kwa mujibu wa ripota wa AFP.

Maandamano yaliyopita, yalisababisha vifo vya watu 15, wengi wakiwa wakaazi wa jiji kuu Kinshasa.

Serikali kwa mara nyingine, imefunga mtandao ili kuzuia mawasiliano kupitia mitandao ya kijamii lakini pia kuzuia watu kuwasiliana kwa ujumbe mfupi wa simu.

Kanisa Katoliki nchini humo limesema, litaendelea kuandaa maandamano haya hadi pale rais Kabila ambaye alianza kuongoza nchi hiyo mwaka 2001 atakapoondoka madarakani.

Kuna wasiwasi kuwa, Kabila ambaye muda wake wa kukaa madarakani ulimalizika mwaka 2016, anaweza kuwania tena wakati wa Uchaguzi Mkuu mwezi Desemba.

Tume ya Umoja wa Matiafa nchini DRC Monusco imeomba serikali ya nchi hiyo kuendesha uchunguzi wa kina kuhusu matukio hayo.