KENYA-SOMALIA-AL SHABAB

Magaidi 23 wa Al Shabab wauawa baada ya kushambuliwa na wanajeshi wa AMISOM

Wanajeshi wa Umoja wa Afrika AMISOM nchini Somalia
Wanajeshi wa Umoja wa Afrika AMISOM nchini Somalia AFP PHOTO/AMISOM/TOBIN JONES

Jeshi la Kenya likishirikiana na lile la Somalia, limewauwa magaidi 23 wa Al Shabab katika mji wa Fahfahdun Kusini Magharibi mwa mkoa wa Gedo nchini Somalia.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti zinasema magaidi hao waliuawa wakati wanajeshi wa Kenya chini ya mwavuli wa AMISOM walipokuwa wanafanya oparesheni ya kulenga ngome mpya za magaidi hao.

Makabiliano makali yalishuhudiwa kwa muda wa saa nne kati ya wanajeshi wa AMISOM na magaidi hao waliokuwa wamejihami kwa silaha hatari.

Majeshi ya Kenya KDF na yale ya Somalia SDF, yanasema mbali na mauaji hayo, walifanikiwa kuwapokonya magaidi hao silaha na kuteketeza moto magari kadhaa pamoja na kambi yao.

Kundi la Al Shabab linasalia hatari kwa usalama wa nchi jirani hasa Kenya lakini pia serikali ya Mogadishu.

Kenya ilituma jeshi lake nchini Somalia mwaka 2011, baada ya Al Shabab kuwateka nyara wafanyikazi wawili wa Kihispania waliokuwa wanalifanyia kazi Shirikila la Madaktari wasiokuwa na mipaka MSF, katika kambi ya Daadab.