DRC-USALAMA

Serikali ya DRC kuwachukulia hatua kali polisi wanaoua waandamanaji

Polisi wakabiliana na waandamanaji karibu na Kanisa kuu la Notre Dame huko Kinshasa, DRC tarehe 25 Februari 2018.
Polisi wakabiliana na waandamanaji karibu na Kanisa kuu la Notre Dame huko Kinshasa, DRC tarehe 25 Februari 2018. REUTERS/Goran Tomasevic

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inasema, itaendelea kuwachukulia hatua maafisa wa usalama watakaobainika kuwauwa waandamanaji kwa kuwapiga risasi.

Matangazo ya kibiashara

Kauli hii imekuja baada ya Mahakama ya Kijeshi hapo jana kumfunga jela afisa wa Polisi maisha jela kwa kumpiga risasi na kumuua mwanadamanaji katika eneo la Mbandaka siku ya Jumapili iliyopita.

Wanaharakati kadhaa wa haki za binadamu huko Mbandaka wamesema wanasikitishwa na namna kesi hiyo ilivyoendeshwa, wakisema kuwa ilikuwa na lengo la kulinda wahalifu halisi wa mauaji hayo.

Hayo yanajiri wakati ambapo polisi mjini Kisangani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imesema kuwa imewaachilia huru Makasisi watatu wa Kanisa Katoliki waliokamatwa siku ya Jumapili iliyopita, wakiongoza maandamano ya kumshinikiza rais Joseph Kabila kujiuzulu.

Polisi nchini DRC imekua ikilaumiwa kutumia nguvu za kupita kiasi kwa kutawanya maandamano hayo.

Watu kadhaa wameuawa tangu maandamano hayo kuanza nchini DRC.