DRC-ITURI-MAUAJI

Watu 50 wauwa jimboni Ituri nchini DRC

Picha ya eneo la Ituri nchini DRC
Picha ya eneo la Ituri nchini DRC MONUSCO/Abel Kavanagh

Watu hamsini wameuawa baada ya watu waliokuwa wamejihami kwa silaha kuvamia vijiji vitatu katika mkoa wa Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti za kijeshi zinasema kuwa mauaji hayo yalitokea Kaskazini mwa eneo la Bahema. Pamoja na mauaji hayo, nyumba za wakaazi wa kijini hicho zilichomwa moto.

Gavana wa Ituri Jefferson Abdullah Penembaka  amelaani mauaji hayo na kusema, hayakubaliki.

Aidha, ametoa  wito kwa wanajeshi wa FARDC kuwatafuta na kuwachukulia hatua wauaji hao.

Mbali na kutumia bunduki kuwashambulia, raia hao wasiokuwa na hatia wakiwemo watoto na wanawake 16, watu hao pia walitumia visu kuwadunga kwa mujibu wa Gavana Penembaka .

Haya sio mauaji ya kwanza katika jimbo hili ambapo raia wasiokuwa na hatia wamekuwa wakivamiwa na makundi ya waasi, lakini pia wakati mwingine mapigano ya kikabila kwa sababu ya ardhi.

Mauaji kama haya yamewaacha maelfu ya wakimbizi nchini DRC.