BURKINA FASO-UGAIDI-UFARANSA

Serikali ya Burkina Faso yashuku wavamizi walishirikiana na jeshi kutekeleza mashambulizi

Wanajeshi wa Burkina Faso wakilinda usalama katika eneo liloshambuliwa
Wanajeshi wa Burkina Faso wakilinda usalama katika eneo liloshambuliwa Ahmed OUOBA / AFP

Duru za serikali nchini Burkina Faso zinasema mtu mmoja anayedaiwa kupanga mashambulizi ya hivi majuzi jijini Ouagadougou katika Ubalozi wa Ufaransa na Makao Makuu ya Jeshi, alipata msaada wa jeshi la serikali.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa hiyo imeeleza kuwa washambuliaji walipewa taarifa muhimu kutoka jeshini, zilizowasaidia katika tukio hilo.

Hata hivyo, serikali ya Burkina Faso inasema kuwa inaendelea kuchunguza tukio hili na itawachukulia hatua wale wote waliohusika.

Kundi la kijihadi linaloshirikiana na kundi la al-Qaeda limedai kuhusika katika mashambulizi hayo.

Wanajeshi wanane waliuawa na wengine 12 kujeruhiwa katika makabiliano na wapiganaji wa kundi hilo la kijihadi linaloojiita GSIM.

Taarifa za kijeshi kutoka Ufaransa zinasema, wanajihadi 20 waliuliwa katika makabiliano hayo.

Ufaransa imesema, mashambulizi hayo yalilenga maslahi ya Ufaransa nchini Burkina Faso.

Paris imetuma kikosi chake cha wanajeshi 4,000 katika nchi za Sahel ambazo ni Burkina Faso, Niger, Mauritania, Chad na Mali kupambana na makundi ya kigaidi.