DRC-UN

Baraza la walei DRC laitaka UN kusimama kidete kuelekea uchaguzi wa Desemba

Baadhi ya maaskofu wa kanisa katoliki nchini DRC.
Baadhi ya maaskofu wa kanisa katoliki nchini DRC. Photo MONUSCO/ John Bompengo

Kamati ya Walei wa kanisa katoliki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametoa wito kwa umoja wa Mataifa kuimarisha wajibu wake wakati wa uchaguzi mkuu wa mwezi Desemba mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Kamati hiyo ya kuratibu shughuli za baraza la Maaskofu ambayo imekuwa ikiitisha maandamano dhidi ya rais Joseph Kabila, imesema inauomba umoja utoe rasilimali za kutosha kwa tume yake nchini DRC kwa lengo la kuwalinda raia kabla na baada ya uchaguzi.

Katika barua yake kwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa Antonio Guterres, kamati hiyo imesema inataka Serikali ya rais Kabila itekeleze matakwa kadhaa ikiwemo kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa na kuachana na kesi zinazowakabili wanasiasa wa upinzani ifikapo Aprili 30 mwaka huu.

kamati hiyo inasema itaahirisha maandamano hadi kwenye tarehe hiyo lakini watalazimika kuyapanua na kuyafanya ya nchi nzima ikiwa mapendekezo yao hayatatekelezwa.

Kamati hiyo pia inataka kuondolewa kwa makataa ya kuzuia maandamano iliyowekwa na Serikali baada ya awali kuzuiwa kwa maandamano yao karibu matatu iliyokuwa imeitisha tangu mwezi Desemba mwaka jana.

Mwezi February mwaka huu chama kikuu cha upinzani nchini DRC, UDPS kiliunga mkono maandamano dhidi ya rais Kabila yaliyoitishwa na baraza la maaskofu.

Utawala wa rais Kabila unakosolewa kwa vitendo vya rushwa, ukandamizaji na ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya waandamanaji.

Tangu kumalizika kwa muhula wake mwezi Desemba mwaka 2016 rais Kabila bado ameendelea kusalia madarakani licha ya makubaliano ya kisiasa yaliyotaka kuundwa kwa Serikali ya mpito.

Mkataba uliosimamiwa na baraza la maaskofu mwaka 2016 ambao ulitaka kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwaka 2017, haukufanikiwa baada ya Serikali kudai kuwa haikuwa na fedha za kuandaa uchaguzi na kutokamilika kwa usajili wa wapiga kura.

Barua ya Walei pia inataka rais Kabila atangaze kutowania urais wakati wa uchaguzi wa Desemba 23 mwaka huu.