NIGERIA-AMNESTY INTERNATIONAL

Amnesty: Vikosi vya Nigeria havikufanyia kazi taarifa za kutekwa kwa wasichana wa Dapchi

Baadhi ya wasichana wa Chibok wanaoendelea kushikiliwa mateka na Boko Haram
Baadhi ya wasichana wa Chibok wanaoendelea kushikiliwa mateka na Boko Haram REUTERS/Zanah Mustapha

Jeshi la Nigeria linatuhumiwa kwa kudharau taarifa za mara kwa mara zilizokuwa zikitolewa kuhusu mwenendo wa wapiganaji wa kundi la Boko Haram kabla ya kutekwa nyara kwa wasichana 110 wa shule kaskazini mwa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Wanafunzi hao ambao mdogo kati ya wote alikuwa na umri wa miaka 10 walitekwa nyara kutoka kwenye mji wa Dapchi jimboni Yobe Februari 19 mwaka huu katika tukio lililofanana kabisa na lile la Chibok.

Wakati ule zaidi ya wasichana 200 wa shule walitekwa nyara katika shambulio ambalo liliibua kilio cha dunia kutafutwa kwa wasichana hao na hatari ya kundi hilo la kiislamu.

Rais Muhammadu Buhari amesema tukio la Dapchi ni janga la kitaifa na kuapa kutumia wataalamu zaidi kuliko jeshi katika kuhakikisha wasichana hao wanaachiwa huru.

Lakini kama tukio la Chibok miaka minne iliypita, shirika la kimataifa linalotetea haki za binadamu Amnesty International limedai kuwa jeshi lilipewa taarifa kuhusu kuwasili kwa wapiganaji hao waliojihami kwa silaha na bado likashindwa kuchukua hatua stahiki.

Katika saa chache zilizopelekea matukio yote mawili mamlaka nchini humo bado zilitoa taarifa kukanusha wasichana hao kutekwa nyara, imesema taarifa ya Amnesty International.

Mkurugenzi wa Amnesty International nchini Nigeria Osa Ojigho amesema “hakuna walichojifunza” kutokana na tukio la Chibok na kutoa wito wa kuanzishwa kwa uchunguzi huru kubaini kile alichosema ni uzembe mkubwa wa vyombo vya usalama.

“Kushindwa kwa Serikali kwenye tukio hili lazima kuchunguzwe na matokeo yake kuwekwa wazi kwa uma, na ni muhimu kwa uchunguzi wowote kujikita katika kiini,” amesema mkurugenzi huyo.

Hata hivyo hadi sasa hakuna majibu yoyote yaliyolewa na jeshi kujibu tuhuma za shirika la Amnesty International hata baada ya kutafutwa na shirika la habari la Ufaransa AFP.